Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera: Nipo tayari kufukuzwa Yanga

82198 Zahera+pic Zahera: Nipo tayari kufukuzwa Yanga

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya Yanga kuanza vibaya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri, Kocha Mwinyi Zahera amesema yuko tayari kufukuzwa.

Zahera ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya mashabiki wa klabu hiyo kumrushia chupa za maji katika mchezo wa juzi ambao Yanga ilifungwa mabao 2-1.

Yanga ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ilicheza chini ya kiwango mchezo huo na kuibua hasira za mashabiki wa klabu hiyo ambao walimrushia Zahera chupa za maji wakati akielekea ndani ya vyumba vya kuvalia nguo baada ya mpira kumalizika.

Wakati kocha huyo akielekea vyumbani, mashabiki wa Yanga walipaza sauti wakimtaka ajiuzulu kwa matokeo mabaya iliyopata. Timu hiyo sasa ina mlima mrefu kupindua matokeo ugenini kwani itahitaji ushindi wa mabao kuanzia 2-0.

Yanga itacheza mchezo wa marudiano na Pyramids Novemba 3, mechi ambayo haitoi matumaini kwa Yanga kusonga mbele katika mashindano hayo.

Pamoja shutuma hizo, Zahera alisema hatishwi na kauli za mashabiki na yuko tayari kuondoka Yanga endapo uongozi wa klabu hiyo utasitisha mkataba wake unaomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Akizungumza na gazeti hili jana, Zahera alisema endapo viongozi wake wataona inafaa aondoke kufuatia timu hiyo kutocheza kwa kiwango bora atabeba mabegi yake kurejea nyumbani. Alisema pamoja na kurushiwa chupa za maji, amechukulia jambo hilo ni sehemu ya mchezo kwa kuwa mashabiki siku zote wanapenda kuona timu yao ikipata matokeo mazuri.

“Mashabiki ni kawaida yao kuwa wakali siku zote wanataka kuona timu inashinda hawataki kusikia jingine kwahiyo sikushangaa ile hali.

“Mnakumbuka kocha wa Simba alipigwa na makopo kwenye uwanja ule? Baadaye si alikuja kubeba ubingwa, kuna mtu alimtolea maneno makali tena?Hao ndio mashabiki wa soka wako hivyo siku zote,”alisema Zahera.

Kocha huyo raia wa DR Congo, alisema hana dhamira ya kuacha kazi, lakini akifukuzwa hatakosa timu ya kufundisha.

Pyramids

Wakati mashabiki wakimtolea macho, Zahera alidai Yanga haina kikosi bora kama Pyramids ingawa amesifu kazi nzuri ya wachezaji wake katika mchezo huo.

“Watu lazima wakubaliane na ukweli hatukuwa katika kiwango sawa na Pyramids, kuna eneo kubwa tumepishana ni vyema tukaangalia timu yetu,”alisema Zahera.

Kocha huyo wa zamani DC Motema Pembe ya DR Congo alisema anajivunia timu bora inayoundwa na wachezaji hodari akiwataja kwa uchache Sadney Urkhob na Juma Balinya.

“Siwezi kukubali timu sio bora angalia mfano Sadney ametoka Thailand huko kuna ligi mbovu? Haya Juma (Balinya) ametoka Uganda huko kuna ligi mbovu kushinda ya hapa? “Angalia leo (jana) nilikuwa nangalia mitandao na makundi ya Whatsap wengi wanampongeza Sadney lakini huyu ndiye mchezaji alikuwa anapigiwa kelele juzi tu Molinga alifunga mabao 15 msimu uliopita,”alidai kocha huyo.

Yanga

Licha ya kushutumiwa kuhusu kiwango kibovu cha Yanga, Zahera alisema kabla ya mchezo alifanya maandalizi yote na kila mchezaji alipewa majukumu yake ndani ya uwanja.

Alisema baada ya kuisoma Pyramids, alitoa maelekezo kwa wachezaji wake kucheza kwa nidhamu kwa kuwa wapinzani wao wanacheza pasi nyingi ingawa wanabadilika kwa pasi ndefu wanapocheza kwenye viwanja vyenye changamoto kama CCM Kirumba.

“Sikutaka kumtumia Makame kwa kuwa kiwango chake kilikuwa chini tangu ametoka timu ya Taifa, nafasi ya kiungo tulipanga kumtumia Feisal Salumu na Kabamba Tshishimbi na ushambuliaji Sadney Urikhob na Juma Balinya.

Alisema mkakati wake katika mchezo ujao ni kucheza kwa kufunguka na lolote linaweza kutokea kwa kuwa anaamini ana kikosi bora huku akisifu kazi nzuri ya Abdulaziz Makame.

Mchezo wa marudiano

Rekodi za mechi za ugenini Yanga inapocheza dhidi ya timu za Kaskazini mwa Afrika, zinaiweka katika nafasi finyu ya kuitoa Pyramids Novemba 3.

Rekodi zinaonyesha katika mechi 10 za mwisho ilizocheza ugenini dhidi ya wapinzani wake, imetoka sare mara moja na kupoteza mechi nane, ikifunga mabao mawili na kufungwa 18.

Pluijm, Kim wafunguka

Wakati Zahera akiwekwa kikaangoni makocha Kim Poulsen na Hans der Pluijm wamesema wako tayari kuinoa Yanga kujaza nafasi ya Zahera endapo ataondolewa. Kim aliyewahi kuifundisha Taifa Stars alisema lolote linaweza kutokea kuhusu kuinoa Yanga.

“Kwa muda huu sina mpango wa kurejea Tanzania, lakini kuhusu suala la Yanga sote hatujui nini kitatokea mbele. Nipo tayari kuzungumza na viongozi wao kama watanihitaji,” alisema Poulsen.

“Nimesikia timu haina mwenendo mzuri. Katika mpira kuna nyakati ambazo lazima timu ipitie, inahitaji nguvu ya ziada kupita salama hasa kipindi ambacho matokeo huwa tofauti na matarajio,” alisema Pluijm.

Chanzo: mwananchi.co.tz