Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera, Aussems waanika silaha

41970 Pic+simba+yanga Zahera, Aussems waanika silaha

Sat, 16 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Moro. Wakati Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera akitambia safu ya ushambuliaji, Patrick Aussems amesema atatumia mbinu kama aliyotumia dhidi ya Al Ahly kuwaangamiza wapinzani wao.

Yanga na Simba zinatarajiwa kucheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaofanyika kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, makocha hao kila mmoja aliweka hadharani mbinu zake kitendo ambacho ni sawa na kumuuzia silaha mpinzani wako.

Akizungumza kwenye mazoezi ya Yanga mkoani Morogoro, Zahera alisema amebaini udhaifu wa Simba na tayari ameandaa mbinu ya kupata mabao katika mchezo huo.

Zahera alisema moja ya maeneo yaliyokuwa yakimpa taabu kupata ushindi ni aina ya upigaji wa mipira ya adhabu na kona ambayo katika mazoezi ya jana asubuhi alitumia muda mrefu kuwapa mafunzo.

“Eneo ambalo limekuwa likitupa shida muda mrefu ni kupiga vizuri mipira ya adhabu na kona tunapokuwa ndani ya eneo la hatari la wapinzani wetu,” alisema Zahera.

Katika mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Highlands, Zahera alikuwa makini akiwataka mabeki wake kuokoa mipira yote ya kona na alikuwa mkali walipokosea.

Jicho la Zahera lilikuwa kwa beki chipukizi wa kulia Paul Godfrey ambaye mara kwa mara alikumbana na kauli kali ya kocha huyo raia wa DR Congo.

Pia alimsimamia kikamilifu Ibrahim Ajibu kupiga vizuri mipira ya krosi hasa wanapokuwa ndani ya eneo la hatari la wapinzani.

Kwa upande wake Aussems alisema kuwa atatumia mbinu kama aliyotumia dhidi ya Al Ahly kuimaliza Yanga.

Aussems alisema atatumia matokeo ya Al Ahly kuilaza Yanga kwa kuwa wachezaji wako vizuri kisaikolojia.

“Tunatoka kushinda mechi muhimu na ngumu dhidi ya Al Ahly morali hiyo ni silaha muhimu katika mechi hii ya Yanga,” alisema Aussems. Simba iliichapa Al Ahly bao 1-0, Dar es Salaam.

Aussems alisema anaiheshimu Yanga ni timu bora inaongoza ligi na wametoka kushinda mechi muhimu ugenini, lakini Simba inahitaji ushindi.

Yanga iliichapa JKT Tanzania bao 1-0, katika mchezo wa ligi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Aussems raia wa Ubelgiji alidai ataingia na mbinu ya kufunguka kwa kucheza soka ya kushambulia ili kupata mabao.

“Tunakwenda kuwashambulia hatutajilinda, tulijaribu kufanya hivyo katika mechi ya kwanza na Al Ahly tukapoteza vibaya tutacheza soka letu la kushambulia, pia tutakuwa imara katika ulinzi.

“Tunakutana na Yanga siwezi kusema wana mapungufu gani hiyo ni siri yangu na wachezaji wangu tukiwa kambini lakini ni timu ambayo narudia tunaiheshimu kwa ubora wao,” aliongeza Aussems.

Pia kocha huyo alizungumzia kuanza vizuri kwa beki wake wa kulia Zana Coulibaly akisema ana matumaini ataisaidia Simba msimu huu.

“Awali, nilisema Zana ni beki imara, lakini mengi yalizungumzwa bila kuzingatia muda alikuja wakati ambao tumetoka kumpoteza Kapombe,” alidokeza Aussems.

Khatimu Naheka, Oliver Albert, Thomas Ng’itu

Chanzo: mwananchi.co.tz