Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yondani, Chirwa watikisa usajili

8931 Usajili+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati kundi kubwa la nyota wa Yanga wakiwa wamemaliza mikataba huku wengine wakipiga hesabu za kuondoka, beki Kelvin Yondani na mshambuliaji Obrey Chirwa ndio wachezaji pekee wenye nafasi kubwa ya kuvuna kiasi kikubwa cha fedha katika msimu huu wa usajili kuliko wengine.

Kiwango bora kilichoonyeshwa na nyota hao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika, kimewafanya wageuke lulu katika kipindi hiki cha usajili na kuwapiga bao mastaa wengine wanane ambao mikataba yao na Yanga imemalizika kama ilivyokuwa kwa wawili hao.

Vyovyote itakavyokuwa Yanga italazimika kutenga kiasi kikubwa cha fedha kuwapa Yondani na Chirwa ili wakubali kutia saini mikataba mipya, lakini hata ikishindwa kuwashawishi wabaki, bado klabu zinazotaka saini zao hasa Simba na Azam zitalazimika kuandaa fungu la kutosha ili kuwanasa.

Hata hivyo, Yanga huenda isilazimike kutumia fedha nyingi kuwashawishi, Geofrey Mwashiuya, Andrew Vincent, Beno Kakolanya, Hassani Kessy, Matheo Antony, Pato Ngonyani, Said Juma ‘Makapu’ na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Chirwa amekuwa tegemeo kwa safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo licha ya kulegalega katika msimu uliomalizika, mshambuliaji huyo pekee ameifungia mabao 13 huku akiwa chanzo cha kupatikana kwa mengine ambayo yamefungwa na klabu hiyo.

Yanga imekuwa ikihaha kumshawishi Chirwa aongeze mkataba mpya na huenda ikampa dau kubwa kwa kuwa tayari anahusishwa na mpango wa kutua Azam au kucheza soka nchini Misri.

Pia Yondani ambaye amekuwa uti wa mgongo wa safu ya ulinzi ambayo licha ya Yanga kuyumba msimu uliomalizika ikishika nafasi ya tatu, lakini libero huyo alikuwa moto wa kuotea mbali.

Yondani ana uwezo mkubwa wa kukabiliana na washambuliaji machachari wa timu pinzani, kutokana na matumizi mazuri ya akili na nguvu aliyonayo anapochuana nao kuwania mpira.

Beki huyo wa kati pia anabebwa na uwezo mzuri wa kuokoa mipira ya juu na kuwapanga wenzake akiwa kiongozi hodari uwanjani.

Ukiondoa Yondani na Chirwa, wengine ambao wanaweza kuvuna fedha ni mabeki Andrew Vincent na Kessy ambao katika siku za hivi karibuni wameonekana kuimarika na kuwa msaada wa safu ya ulinzi.

Wachezaji wengine waliobaki wanaonekana kutowaumiza kichwa Yanga, kwa sababu wanacheza katika nafasi ambazo wapo nyota wanaocheza na kufanya vizuri zaidi yao. Pia hawana uhakika wa nafasi kwenye kikosi cha Yanga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika alisema hakuna mchezaji muhimu ambaye ataondoka kwenye klabu hiyo na amewataka wanachama na mashabiki kuwa watulivu.

“Nawaomba Wanayanga kuwa watulivu, kamati ya usajili tumejipanga kikamilifu kuhakikisha wachezaji wetu wote tunaowahitaji hawaendi kokote. Tayari tumeanza mazungumzo na wachezaji yapo kwenye hatua nzuri,” alisema Nyika.

Tofauti na Simba ambayo imeanza usajili wa kishindo kwa kunasa nyota watatu wakali Adam Salamba (Njombe Mji), Marcel Kaheza (Majimaji) na Mohammed Rashind kutoka Tanzania Prisons, Yanga imepoa.

Klabu hiyo imeshindwa kuonyesha makeke ya usajili baada ya kuyumba kiuchumi hatua iliyochangia wachezaji kukosa mishahara ya miezi kadhaa.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, amekiri kuwa klabu hiyo inapitia kipindi kigumu baada ya kukumbwa na mtikisiko wa kiuchumi.

Mkwasa ambaye ni kocha mkongwe, amesema wanapambana kuhakikisha Yanga inafanya usajili mzuri kulingana na mahitaji ya kocha mkuu Mwinyi Zahera.

Chanzo: mwananchi.co.tz