Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yawataka mashabiki 'kupotezea' kipigo

YANGAA Yanga

Thu, 16 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAISHA yaendelee! Yanga imewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kusahau kipigo walichokipata dhidi ya watani zao, Simba na kuelekeza 'akili' katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizobaki ili kumaliza msimu kwenye nafasi ya pili.

Yanga ilichapwa mabao 4-1 na Simba na kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la FA, ambayo bingwa wake atakata tiketi ya kupeperusha bendera ya Bara kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli alisema imekuwa ni bahati mbaya kwao kupoteza mchezo huo dhidi ya Simba ambao umewafanya wapoteze nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa msimu ujao.

Bumbuli alisema Yanga imepoteza mechi lakini haijapoteza heshima ya klabu yao ambayo inarekodi ya kushinda mataji mbalimbali.

"Tumepoteza mchezo, tumepoteza nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho, lakini hatujapoteza thamani ya klabu ya Yanga na heshima yetu, ndiyo maana ya kauli yetu ya daima mbele nyuma mwiko, yale yote yameshapita, tunaganga yajayo, lengo letu ni kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu," alisema Bumbuli.

Kiongozi huyo amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kushikamana na kuendelea kujenga hamasa kuelekea katika msimu mpya.

"Kwanza lengo ni kushinda mechi zote zilizosalia ili tushike nafasi ya pili kwa ajili ya heshima ya klabu yetu, huku mengine yote yakifanyiwa kazi kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, pamoja na usajili, lakini kuna maandalizi ya Siku ya Mwananchi ambayo tayari yameshaanza," Bumbuli alisema.

Baada ya Yanga kutolewa katika mashindano ya Kombe la FA, tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika imekwenda kwa Namungo FC ambayo imetinga fainali kutokana na Simba tayari kuwa na tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live