Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amesema makosa ya ndani nan je ya uwanja aliyoyafanya aliyekuwa kocha wake mkuu, Cedric Kaze ndiyo yaliyopelekea kocha huyo kutimuliwa.
Bumbuli ameyasema hayo wakati alipokuwa anafanya mahojiano maalum na East Africa Radio na kugusia kuwa utofauti huo huenda ulipelekea timu hiyo kuwa na mwenendo usioridhisha wa matokeo ndiyo maana ikagharimu kibarua chake.
Bumbuli ameanza kwa kusema “Cedric Kaze alikuwa chaguo sahihi sana kwa klabu ya Yanga. Makosa huwa yanatokea yanafanyika na huwa yanawagharimu watu ikiwemo yeye mwenye. Makosa aliyoyafanya pengine yalikuwa ya nje ya uwanja zaidi ambayo yakagrimu ajira yake."
Cedric Kaze alitimuliwa Yanga Machi 7, 2021 baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha matokeo ambayo yalikuwa muendelezo wa kuboronga.
Baada ya miezi sita kupita tokea Kaze atimuliwe, Yanga walimtangaza Kaze Septemba 29, 2021 kuwa amerejea lakini safari hii ni Kocha Msaidizi chini ya Mohammed Nasreddine Nabi ambaye ndiye kocha Mkuu.
Kujibia swali la sababu zilizomrejesha Kaze Jangwani ni zipi? Bumbuli amesema walitafakari na kuona haja ya kutaka kuendeleza project waliozianzisha na kocha huyo pamoja na kumsaidia Nabi kuunda kikosi bora zaidi.
Bumbuli amesema, "Lakini baada ya kukaa na kutafakari kuona kwamba tuna mwalimu mpya lakini tunatafuta mwalimu ambaye atakuja kuendeleza falsafa ile ambayo tulikuwa tunayo na tunaihitaji kama Young Africans, taukasema Okay tunakasema tuna nafasi nzuri pia tunaweza kumwambia kaaze”.
"Mwalimu yalitokea haya na haya ambayo tunaamini tunaweza tukarekebisha, unaweza kuwa msaidizi wa Kocha Naby? Ili zile mambo yetu tuliyokuwa tumeyapanga yaweze kukamilika licha ya haya yote kutokea".
"Na hakuna jambo zuri kama watu kuachana vizuri. Tuliachana na Mwalimu kazi vizuri, na akaona anaipenda Yanga, ni mtu ambaye anaipenda kazi yake akasema yeah nilikuwa na wakati mzuri Tanzania, nilikuwa na wakati mzuri na mashabiki wa Yanga, yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Tuka negotiate package akakubali akaja."
Tokea arejee Yanga, Kaze amehudumu akiwa kocha msaidizi kwenye michezo yote miwili ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania na kuisaidia Yanga kupata ushindi wa 1-0 kwenye michezo yote miwili na Yanga kushika nafasi ya pili kwenye msimamo licha ya kuwa na alama sawa na Kinara, Polisi Tanzania.