Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yatamba haishikiki

102382 Pic+yanga Yanga yatamba haishikiki

Thu, 2 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wao Mbelgiji afunguka wanalihitaji zaidi Kombe la FA, amwondoa Morrison katika mipango yake...

TUNALIHITAJI! KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amewataka wachezaji wake kuachana na matokeo ya mechi iliyopita, na badala yake kuweka nguvu kwenye mechi ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA bila kujali watakutana na nani.

Yanga ilifanikiwa kusonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuwaondoa Kagera Sugar kuwafunga mabao 2-1 katika mchezo wa hatua ya robo fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Yanga sasa itakutana na mshindi wa mchezo wa robo fainali nyingine ya mwisho inayowakutanisha Simba dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Azam FC.

Akizungumza na gazeti hili jana, Eymael alisema haikuwa kazi rahisi kusonga mbele, hivyo wanahitaji kuongeza nguvu ili wafanye vizuri katika mchezo wa hatua inayofuata.

Eymael alisema anawapongeza wachezaji wake kwa morali waliyoionyesha kwenye mechi hiyo licha ya kutanguliwa kufungwa bao, na kuwataka waendelea kujituma ili wafikie malengo.

"Nawapongeza wachezaji wangu kwa namna walivyopambana, kwa sasa nataka walekeze mawazo yao kwenye michezo mingine, huu (dhidi ya Kagera Sugar) umepita, FA ndio kombe ambalo tunalipigia mahesabu kwa sasa," alisema Eymael.

Mbelgiji huyo aliongeza jambo kubwa ambalo liko mbele yao ni kuhakikisha wananyakua kombe hilo ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

"Tuna michezo imebaki ya ligi, lakini kwa sasa Kombe la FA ni muhimu zaidi, kwa sababu tayari ligi ni kama imeisha kwa sababu bingwa ameshapatikana, mashabiki waendelee kutusapoti na sisi tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye FA.

"Nipo tayari kukutana na Azam au Simba ambao ni mabingwa, tutacheza vizuri, nina imani tukikutana utakuwa mchezo nzuri na wenye ushindani mkubwa, tumejipanga kulichukua kombe hilo, ndio malengo na mikakati tuliyonayo," Eymael aliongeza.

Aliweka wazi anatamani zaidi kukutana na Simba katika hatua hiyo inayofuata na anaamini mchezo utakuwa mzuri kwa sababu watani zao hao hucheza mpira mzuri na wakuvutia kila wanaposhuka uwanjani.

Kocha huyo alisema amechukizwa na kitendo cha utovu wa nidhamu ulionyeshwa na kiungo mshambuliaji wake, Bernard Morrison kwa kutoroka kambini.

Alisema hataki kusikia habari za mchezaji huyo pia amemwondoa katika mipango yake kwa sasa kutokana na tabia hiyo aliyoionyesha wakati timu yao ikiwa kwenye 'vita' ya kusaka nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

"Sitamjumuisha katika kikosi changu endapo atarudi, kitendo cha kuondoka bila ruhusa ni utovu wa nidhamu ambao hakuna mtu atakubaliana na tabia hiyo," alisema Eymael.

Alieleza mchezaji anayejitambua hawezi kuondoka kambini wakati timu yake ina mechi ngumu ya kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kushindwa kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

"Hii ni nafasi hatutaki kupoteza, Yanga sio ya mchezaji mmoja, tunapopata ushindi ni wetu sote, kila mmoja tunasimama katika mstari mmoja kufikia malengo yetu," kocha huyo aliongeza.

Mkongomani, David Molinga na Deus Kaseke walifunga mabao kwa upande wa Yanga wakati goli pekee la Kagera Sugar lilipachikwa wavuni na Awesu Awesu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live