Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yasuka ukuta wa chuma

11627 Pic+yanga TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Kambi ya siku 12 ambayo Yanga imeweka mkoani Morogoro, imeipa timu hiyo safu imara ya ulinzi ambayo inaamini itazima vishindo na mbwembwe za Simba na Azam zilizosajili washambuliaji wa gharama kubwa.

Simba na Azam kila moja imetumia zaidi ya Sh150 milioni kunasa saini za wachezaji kama Donald Ngoma, Dan Lyanga, Tafadzwa Kutinyu, Ditram Nchimbi, Meddie Kagere, Mohammed Rashid, Marcel Kaheza na Cletus Chama tofauti na Yanga ambayo haijatumia gharama kubwa.

Benchi la ufundi Yanga limefanya tathmini ya kina kwa vikosi vya wapinzani wake na kubaini kuwa njia ya kwanza itakayosaidia kupambana na Simba, Azam ni kusuka safu imara ya ulinzi ambayo itahakikisha washambuliaji wa timu hizo hawafui dafu watakapokutana.

Ukuta huo wa chuma ambao Kocha Mwinyi Zahera ameusuka kwa ajili ya msimu ujao, unaundwa na mabeki watano ambao huenda watakuwa wakianza kwa pamoja tofauti na ule wa mabaki wanne ambao Yanga imekuwa ikitumia mara kwa mara.

Mabeki hao watano ambao watakuwa na jukumu la kumlinda kipa Klause Kindoki mwenye nafasi kubwa ya kuwa chaguo la kwanza la Yanga ni Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondani na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Hata hivyo, Ninja atakuwa akisimama mbele kidogo ya mabeki wanne, mbinu ambayo inaonekana inalenga kumpa nafasi kutoa usaidizi wa haraka kwa Dante na Yondani katika kutibua mashambulizi.

Mabeki hao watano watasaidiwa na kiungo Papy Tshishimbi ambaye atakuwa na jukumu la kuunganisha idara ya ulinzi na ushambuliaji huku mbele yake akisimama Feisal Salum ambaye kazi yake itakuwa kuchezesha timu na kutengeneza mashambulizi ya Yanga.

Wakati Heritier Makambo akisimama kama mshambuliaji pekee wa kati, Deus Kaseke na Mrisho Ngassa watakuwa na jukumu la kushambulia kutokea pembeni ingawa kutokana na kasi waliyonayo, watakuwa wakilazimika kushuka kusaidia ulinzi kwa mabeki wa pembeni.

Katika kuhakikisha kuwa anataka kuona timu yake inakuwa na safu imara ya ulinzi msimu ujao, Zahera mara kwa mara amekuwa akisisitiza zaidi wachezaji wake kuwa na pumzi ya kutosha

“Tumekuwa na muda wa kutosha wa kufanya mazoezi. Unajua tulipokuwa Dar es Salaam tulikuwa tunafanya mazoezi mara moja kwa siku. Ile haikuwa ratiba nzuri lakini pia wachezaji wanaenda kula chakula ambacho hukijui na kulala ambako hupajui,”alisema Zahera.

“Tumekuwa kambini mambo yamebadilika. Tumefanya mazoezi ya kutosha, wachezaji wamepumzika vizuri na sasa timu ipo katika ubora sawa na hata zile timu zilizokwenda Uganda na Uturuki.

“Kwa sasa naweza kusema timu imekuwa na ubora tayari kwenda kushindana ingawa bado haijafikia katika kile kiwango ninachotaka, lakini kwa kuwa muda upo kidogo tutamalizia vizuri.” alisema kocha huyo.

Zahera alisema anahitaji kuona wachezaji wanaojituma muda wote uwanjani kwasababu ndio siri ya kufanya vizuri na kushindana kikamilifu na wapinzani wao kwenye mbio za kutwaa ubingwa msimu ujao.

“Timu yangu sihitaji wavivu nahitaji wachezaji wanaokaba na kushambulia kwa kasi ndiyo maana tumefanya mazoezi makali ya kuongeza nguvu ya mwili.

Lengo ni kucheza kwa nguvu,”aliongeza kocha huyo raia wa DR Congo.

Chanzo: mwananchi.co.tz