Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yarudi mikononi mwa Lipuli nusu fainali ya Kombe la FA

49701 Yanag+pic

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza: Yanga inarudi tena mikononi mwa Lipuli FC baada ya jana kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuichapa Alliance FC penalti 4-3 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Lipuli iliifunga Yanga bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Machi 16 kwenye Uwanja wa Samora Iringa hivyo ni wakati wa timu hiyo kulipa kisasi katika mchezo huo wa nusu fainali ya FA utakaofanyika kwenye uwanja huo.

Mchezo mwingine wa nusu fainali FA utazikutanisha Azam dhidi ya KMC.

Katika mchezo wa jana, kipa wa Yanga, Klaus Kindoki alikuwa shujaa wa Yanga katika mchezo wa jana baada ya kupangua penalti mbili za Alliance zilizopigwa na Dickson Ambundo na Sirajio Juma hivyo kuwapa furaha wenzake hasa beki Kelvin Yondani na Mrisho Ngassa ambao walikosa penalti zao kwa upande wa Yanga.

Mashabiki wa Yanga wamekuwa hawana imani na Kindoki na kumuona kama kipa wa kawaida lakini kadri siku zinavyokwenda amekuwa akiwadhihirishia uwanjani kwa kucheza kwa ubora mkubwa hivyo kukazia maneno ya kocha wake, Mwinyi Zahera ambaye alitaka watu kumpa muda kipa huyo kwani ni mchezaji mzuri na sio kumbeza kama wanavyofanya.

Mchezo huo ilibidi kwenda hatua ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.

Mchezo ulivyokuwa

Timu zote zilianza mchezo huo kwa kasi lakini Alliance walionekana wako vizuri zaidi dakika 30 za kipindi cha kwanza huku wakiwabana vilivyo Yanga.

Yanga ililishambulia lango la Alliance kama nyuki na kupata bao dakika ya 38 lililofungwa na Heritier Makambo.

Makambo alifunga bao hilo kwa shuti kali lililogonga mwamba wa pembeni ya goli na kutinga nyavuni kisha kutoka nje baadaya nyavu hizo kuchanika.

Hata hivyo, Alliance walisawazisha bao hilo dakika ya 61 kupitia kwa Joseph James kwa kichwa akimalizia mpira wa faulo uliopigwa na Mapinduzi Balama.

Baada ya dakika 90 za mwamuzi Florentina Zabloni aliamuru mikwaju ya penalti ambayo ya Yanga ilifungwa na Paul Godfrey, Thaban Kamusoko, Haruna Moshi ‘Boban’ na Deus Kaseke huku Kelvin Yondani na Mrisho Ngassa wakikosa.

Waliofunga kwa upande wa Alliance ni Joseph James, Geofrey Luseke na Sameer Vincent wakati Martin Kigi, Dickson Ambundo Siraji Juma walikosa penalti zao.



Chanzo: mwananchi.co.tz