KIKOSI cha Yanga kimerejea jijini Dar es Salaam kikitokea Mbeya na wachezaji wakapewa mapumziko kabla ya kuanza kuwawinda watani wao Simba.
Yanga imerejea leo asubuhi ikitokea Mbeya ilipowachapa wenyeji wao Mbeya Kwanza na kuzidi kujikita katika kilele cha msimamo wa Ligi Kuu Bara wakifikisha pointi 19 baada ya kucheza mechi 7.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa amesema katika kikao cha benchi la ufundi na wao kama uongozi wamekubaliana kuwapa mapumnziko ya siku mbili wachezaji wao baada ya ushindi huo.
Senzo amesema baada ya mapumziko hayo kikosi chao haraka kitarejea kambini kuanza maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya Simba utakaopigwa Desemba 11 katika Uwanja wa Mkapa.
"Tumeona wachezaji nao wakazione familia zao katika hizi siku mbili na baada ya mapumziko hayo tutarejea kazini kuanza kujipanga na mchezo huo unaokuja dhidi ya watani wetu Simba,"amesema Senzo.
Aidha Senzo amesema kuanzia uongozi wao,wachezaji na makocha wanatamani matokeo ya ushundi katika mechi hiyo kubwa inayokuja na kwamba maandalizi yao yatakuwa yenye uzito unaostahili.
"Achana na sisi viongozi wachezaji wetu wanajua umuhimu wa ushindi katika mechi hii na hata makocha wao kwahiyo tutakuwa na maandalizi yanayolingana na uzito wa hii mechi tunakiamini kikosi chetu."