Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yapata 'pigo' lingine

100531 Yanga+pic Yanga yapata 'pigo' lingine

Fri, 26 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

***Beki wake kisiki afungiwa mechi tatu, huku kocha Mbelgiji akilalamika washambuliaji wanamwangusha...

WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, akiwatupia lawama washambuliaji wake kwa kushindwa kutumia nafasi walizozitengeneza katika mchezo dhidi ya Namungo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, beki wake wa kati, Lamine Moro amefungiwa kucheza michezo mitatu.

Adhabu hiyo imekuja siku chache baada ya winga wao, Bernard Morrison kufungiwa mechi mbili pamoja na kutozwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na kufanya vitendo visivyokuwa vya kiungwana.

Lamine pia amepigwa faini ya Sh. 500,000 na Bodi ya Ligi.

Eymael aliliambia gazeti hili baada ya mchezo huo kumalizika kuwa washambuliaji wake ndio walioinyima timu hiyo ushindi kwa sababu ya kutokuwa makini kwa kupoteza nafasi nyingi hasa dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Mbelgiji huyo alisema washambuliaji wake wangekuwa makini na kutumia vema nafasi walizopata, ana imani wangeenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3-1.

"Nimefanya kazi yangu ipasavyo, ila bado kazi kubwa ipo kwa washambuliaji, kukosa nafasi nyingi za wazi kwa kutokuwa makini," alisema Eymael.

Kocha huyo alisema hajafurahishwa na matokeo hayo ambayo yanawaweka kwenye wakati mgumu wa kumaliza msimu katika nafasi ya pili ambayo inawaniwa pia na timu nyingine ikiwamo Azam FC.

"Wachezaji wamepambana ila kuna jambo linalishangaza, na hili lipo hapa Tanzania kwa uamuzi unaofanywa na waamuzi," Eymael alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania, Almasi Kasongo, alisema katika taarifa yake Lamine amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la kumkanyaga mchezaji wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto katika mechi iliyochezwa Juni 17, mwaka huu jijini Dodoma.

"Kamati imeiomba Yanga kukaa na mchezaji wao huyo (Lamine), kumkumbusha kuhusiana na mchezo wa kiungwana anapokuwa kwenye majukumu ya kuitumikia klabu hiyo," Kasongo alisema.

Aliongeza Bodi ya Ligi imepeleka malalamiko ya Azam FC kuhusu uamuzi uliofanywa katika mchezo wao dhidi ya Yanga katika Kamati ya Waamuzi.

"Katika malalamiko yao, Azam wamedai walipaswa kupewa mabao mawili na penalti moja baada ya mchezaji wao kuangushwa ndani ya eneo la penalti," alisema kiongozi huyo.

Alisema pia JKT Mlale ya Songea, imepoteza mchezo wake wa Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Dodoma FC, kwa sababu mashabiki wake walivamia uwanjani na kumshambulia mwamuzi wa kati na mwamuzi msaidizi namba mbili na kusababisha mchezo huo kuvunjika.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 43 (4), ya Ligi Daraja la Kwanza, Dodoma FC inapewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu, huku Mlale ikitozwa faini ya Sh. 500,000 wakati Kocha Msaidizi wa Maafande hao, Rashid Mpenda, akitozwa faini ya Sh. 300,000 na kufungiwa miezi sita kwa kosa la kushambulia waamuzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live