***Lengo ni kuwa na kikosi 'tishio' ambacho kitatoa 'dozi' mfululizo katika msimu ujao...
KATIKA kuhakikisha inarejea katika ushindani wa kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa Yanga ya jijini Dar es Salaam, umejipanga kuhakikisha unafanya usajili wa vitendo wa nyota wenye viwango vya juu wa kimataifa, imeelezwa.
Uamuzi huu unatokana na 'hasira' ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu miwili mfululizo, huku pia ikipoteza matumaini ya kutwaa taji hilo kwa msimu huu wa 2019/20 ambao unaelekea ukingoni.
Tayari wadhamini wa Yanga, Kampuni ya GSM, imetangaza kutenga bajeti ya Sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa usajili wa kikosi cha timu hiyo cha msimu ujao kama ilivyopendekezwa na Kocha Mkuu, Mbelgiji Luc Eymael.
Mkurugenzi Mwekezaji wa GSM, Hersi Said, aliliambia gazeti hili kampuni hiyo imejiandaa kufanya usajili wa 'kishindo' kwa ajili ya msimu ujao na mchakato huo utatekelezwa kwa vitendo hivi karibuni.
Said alisema wanataka kuifanya Yanga kuwa timu inayoogopewa katika msimu ujao baada ya GSM kuchelewa kuingia mkataba wa udhamini hapo mwaka jana.
"Tutafanya usajili wa daraja la juu, wa kiwango kikubwa, hii itawashtua wote wanaoiangalia Yanga, usajili wetu utafanywa kwa utulivu kwa sababu tunajua malengo tuliyoyaweka kwa ajili ya msimu ujao," alisema Said.
Aliongeza katika kuhakikisha Yanga inapata fedha kupitia mauzo ya jezi za wachezaji wake, wako katika maandalizi ya kuandaa mfumo sahihi kwa kushirikiana ili zoezi hilo liwe na mafanikio.
Kiongozi huyo alisema Yanga, GSM inatarajia kushirikiana na idara za serikali ili kuepusha wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kuingiza nchini jezi feki.
"Tunatengeza mfumo mpya ambao utakuwa unatulinda sisi dhidi ya wale wanaohujumu, tutashirikiana kikamilifu na idara za serikali ili zitusaidie katika jambo hili, tunawakumbusha wanachama kufahamu sehemu sahihi wanazotakiwa kwenda kununua jezi," Said alisema.
Aliongeza wanatarajia kuleta bidhaa zenye ubora wa hali ya juu ambazo zitaongeza chachu ya mauzo kwa ajili ya kusaidia klabu hiyo kupata fedha za kujiendesha.
Ukiondoa wachezaji mbalimbali wa kimataifa wanaotajwa kutua nchini kujiunga na Yanga, nyota wa hapa nchini walioko kwenye rada za timu hiyo ni pamoja na mshambuliaji wa Namungo FC, Relliants Lusajo na beki wa kushoto wa Polisi Tanzania, Yassin Mohamed.
“Tangu nilipoanza kusikia tetesi za uongozi kutaka kumsajili Lusajo na Yassin, nimekuwa nikiunga mkono kwa asilimia zote, kwani ni wachezaji wazuri, Lusajo tulishawahi kuwa naye Yanga, hivyo anaifahamu vizuri changamoto zake, ila hata hivyo utaona Yanga ilimwacha si kwa ubaya isipokuwa kocha wa kipindi hicho alikuwa na mastraika wengi, Yassin yeye nilianza kumkubali tangu alipokuwa Ndanda FC, hivyo naujua uwezo wake,” Nahodha Msaidizi wa Yanga, Juma Abdul alisema.
Hata hivyo, bado Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halijafungua rasmi dirisha la usajili na sasa linaendelea na vikao mbalimbali ili kujua hatima ya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili, Ligi Kuu ya Wanawake na mashindano ya Kombe la FA ambayo yalisimamishwa ili kujikinga na virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19).