Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaacha mbili Sokoine

6913 Yanga Logo TZW

Mon, 23 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga jana ilishindwa kutamba mbele ya Mbeya City baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa dimba la Sokoine Mbeya.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa mgumu kwa pande zote, Mbeya City ilionekana kuanza vyema baada ya kuhimili dakika 10 za mwanzo ikipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Yanga.

Pamoja na mashambulizi hayo, timu hiyo ilikosa baadhi ya nafasi za wazi, ambapo mshambuliaji Eliud Ambokile alikosa nafasi mbili za wazi huku akigongesha mwamba kunako dakika ya 21.

Yanga ilionekana kutulia na kuzima mashambulizi hayo huku ikitumia mipira ya pembeni ambayo mpaka mapumziko haikuwa na madhara kwa wapinzani wao.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko ya kumtoa Kelvin Yondan aliyeumia tangu kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na nahodha Nadir Canavaro.

Mpira uliendelea kwa kasi kwa timu zote, lakini Yanga walifanya mabadiliko dakika ya 51 kwa kumpumzisha Emmanuel Martin na kumuingiza Juma Mahadhi.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na tija kwa upande wa timu hiyo ambapo usumbufu wa winga ulifanya mabeki wa Mbeya City kumchezea madhambi na kusababisha adhabu nje kidogo ya eneo la hatari la timu, faulo iliyozaa bao la timu hiyo lililofungwa na kiungo Raphael Daudi dakika ya 57.

Dakika ya 60 mchezo huo uliingia taharuki na kusimama kwa dakika kadhaa, baada ya mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa Mbeya City kumtupia mawe kipa Youthe Rostand na kufanya mchezo usimame kwa muda.

Wakati Yanga ikiendelea kutafuta bao la kujihakikishia ushindi, beki wa Mbeya City, Ramadhani Malima alijikuta akitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Yusuph Mhilu.

Baada ya dakika tisini kukamilika mwamuzi Shomary Lawi aliongeza dakika sita kufidia dakika zilizopotea kwa matukio mbalimbali.

Pamoja na kuwa pungufu dakika hizo za nyongeza, Mbeya City ilionekana kuwa moto ambapo dakika ya 92 ilisawazisha bao hilo kupitia Idd Selamani akipokea pasi ya Kenny Kunambi.

Baada ya matokeo hayo Yanga iliendelea kukaa nafasi ya pili kwa pointi 48 na ikiwa na michezo miwili mkononi.

Chanzo: habarileo.co.tz