Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga washindwe wenyewe CAF

Sun, 22 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga wamepangwa kundi ‘mchekea’ lenye timu za ukanda wa Afrika Mashariki na Algeria.

Katika droo iliyochezeshwa jana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Yanga imepangwa kundi D na timu za Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda na U.S.M Alger ya Algeria.

Timu hizo zote zinafahamiana baada ya kukutana mara kadhaa, Alger ndiyo inaonekana kuwa timu ya tofauti kwenye kundi hilo.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo mechi za raundi ya kwanza zinatarajiwa kuanza mwanzoni mwa Mei ambapo Yanga itaanzia ugenini Algeria kabla ya kucheza na Gor Mahia na kumalizia na Rayon.

Yanga iliingia hatua hiyo ya makundi baada ya kuichapa Wolaita Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1. Gor Mahia ilifuzu baada ya kuitoa Supersports United ya Afrika Kusini kwa bao la ugenini, walishinda nyumbani 1-0 na ugenini wakapoteza 2-1 na Rayon ilishinda 3-0 nyumbani na kufungwa 2-0 ugenini dhidi ya Costa do Sol ya Msumbiji.

Timu nyingine ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Al Hilal ya Sudan imeangukia katika kundi B lenye timu za Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco, El Masry ya Misri na Desportivo do Songo ya Msumbiji.

Aidha, kundi A kuna timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast, Raja Club Athletic ya Morocco, AS Vita ya Congo DR na Aduana Stars ya Ghana. Kwenye kundi C kuna timu za Enyimba ya Nigeria, Williamsville ya Ivory Coast, Club Athletic Renaissance ya Congo na Djoliba AC Bamako ya Mali.

Chanzo: habarileo.co.tz