Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga kuuleta ubabe FA Cup

33171 Pic+yanga Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya timu za Ligi Kuu zikiendeleza nuksi ya kutolewa na zile za madaraja ya chini, Yanga leo inatupa karata yake ya kwanza dhidi ya Tukuyu Stars kwenye mashindano ya Azam Sports Federation Cup.

Mashindano hayo yanayofanyika kwa msimu wa nne tangu yaliporudishwa rasmi, kwa mujibu wa kanuni, bingwa wake ndio huiwakilisha Tanzania Bara kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mabingwa hao wa taji hilo msimu wa 2015/2016 wanapaswa kuingia na tahadhari kubwa ili kukwepa mtego ambao tayari umeshaziumiza timu nne za Ligi Kuu ambazo zimetupwa nje ya mashindano hayo na timu zinazoshiriki madaraja ya chini.

Nuksi hiyo ambayo Yanga wanapaswa kuiepuka leo dhidi ya Tukuyu Stars, ilianzia Ijumaa iliyopita pale Ruvu Shooting ilipochezea kichapo cha mikwaju ya penati 6-5 nyumbani dhidi ya Maafande wa Mighty Elephant kutoka Ruvuma ambayo ipo Ligi Daraja la Pili baada ya timu hizo kumaliza kwa sare ya bao 1-1.

Wakati wengi wakiduwazwa na matokeo hayo, juzi Jumapili, Pan African iliyopo Ligi Daraja la Pili. iliichapa Mwadui FC ya Ligi Kuu kwa mabao 3-1 kama ilivyotokea kwa Mbao FC iliyofungwa nyumbani kwa mikwaju ya penati 4-2 na Dar Ciy ya Ligi Daraja la Kwanza.

Timu nyingine za Ligi Kuu ambazo zinapaswa kuwa darasa kwa Yanga leo baada ya kuchezea vichapo kutoka kwa timu za chini ni Ndanda FC ambayo yenyewe ilitandikwa na Transit Camp iliyopo Ligi Daraja la Kwanza kwa mikwaju ya penati 3-2 nyumbani baada ya timu hizo kwenda sare tasa katika dakika 90.

Yanga pia inapaswa kuingia na tahadhari ikivuta kumbukumbu ya kilichowatokea watani wao wa jadi, Simba msimu uliopita ambao walitolewa hatua kama hii na Green Warriors ya Daraja la Pili.

Pamoja na tahadhari hiyo ambayo Yanga wanapaswa kuingia nayo, huenda leo wakafanya mabadiliko kadhaa kwa kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji wake ambao wamekuwa hawachezi mara kwa mara msimu huu.

Inaweza ikawa nafasi ya kipa Klaus Kindoki kuanza kurudisha imani aliyopoteza mbele ya mashabiki wa Yanga kwa kuanza langoni ili kumpa mapumziko kipa Ramadhan Kabwili ambaye aliumia kwenye mchezo dhidi ya African Lyon.

“Tunaitazama mechi yetu dhidi ya Tukuyu Stars kama moja ya mechi ngumu kwetu kwa sababu mara nyingi timu hizi zinazoonekana ndogo zimekuwa na kawaida ya kukamia pindi wanapocheza na timu za Ligi Kuu.

Na umakini wetu umeongezeka zaidi baada ya kuangalia matokeo ya mechi zilizochezwa juzi ambapo tayari baadhi ya timu za Ligi Kuu zimeshatolewa hivyo tunaipa uzito mkubwa mechi hii na hatuwezi kuwadharau,” alisema mratibu wa Yanga, Hafidh Salehe.

Kule Shinyanga, Stand United wenyewe watakuwa nyumbani kuwakaribisha Ashanti United ‘Watoto wa Jiji’ kwenye mechi itakayochezwa Uwanja wa Kambarage.

Mashindano hayo yataendelea Jumatano wakati Mtibwa Sugar watakapoikaribisha Kiluvya United huku Simba wakiwa nyumbani kucheza na Mashujaa FC ya Kigoma.



Chanzo: mwananchi.co.tz