Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga kumbe haitanii buana

45798 Pic+yanga Yanga kumbe haitanii buana

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

KIKOSI cha Yanga jana Ijumaa kiliendelea na mazoezi yake jijini Dar es Salaam kujiweka tayari kabla ya kuvaana na KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa kesho Jumapili, lakini huku nyuma mabosi wa timu hiyo waliamua kuanika kamati maalum ya kusaka mamilioni ya fedha.

Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe 26 ipo chini ya Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, huku ikiwajumuisha vigogo wengine kadhaa akiwamo Abdallah Bin Kleb, Hussein Ndama na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Joketi Mwegelo ‘Kidoti’.

Lengo la kamati hiyo ni kusaka fedha za usajili wa msimu ujao ndani ya Yanga, iliyoasisiwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera hivi karibuni.

Taarifa kutoka uongozi wa Yanga zinasema kamati hiyo itasimamia zoezi hilo la uchangiaji wa fedha ili kuwezesha usajili wa msimu ujao baada ya msimu huu kufanya usajili wa kuungaunga kwa kukosa fedha hasa baada ya bilionea wao, Yusuf Manji kujiweka kando tangu alipojiuzulu.

Kocha Zahera aliasisi kampeni hiyo kwa kutaka kuunda kikosi bora kitakachofanya vyema msimu ujao akilenga kutafuta kiasi kisichopungua Sh1 bilioni kufanikisha mchakato huo, akiamini kuwa huenda mwakani wakaiwakilisha Tanzania katika michuano ya CAF.

Kikosi kamili cha kamati hiyo ni Mwenyekiti wake ni; Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde akisaidiwa na Lucas Mashauri, huku katibu akiwa Mhandisi Deo Mutta.

Wajumbe wake ni vigogo, Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Hussein Ndama, Hamad Islam, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Athuman Kihamia, Samuel Lukumay, Said Ntimizi, Yanga Makaga, Mussa Katabaro, Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya Kisarawe.

Wengine ni Thobias Lingalangala, Hussein Yahya, Said Mrisho, Issa Kipemba, Debora Mkemwa, Abdulmalik Hassan, Clifford Lugora, Nsubisi Mwasandende, Dk David Ruhago, Pelegrinius Rutayuga, Madaraka Marumbo, Dismas Ten, Omar Kaya na Jimmy Mafufu.

Uzinduzi rasmi wa kamati hiyo unatarajiwa kufanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Mlimani City ambapo mpaka sasa inaelezwa zoezi hilo limeshapokea kiasi kisichopungua Sh 50 milioni.

YAIPIGIA HESABU KMC

Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema mechi yao ya kesho wanaichukulia kwa uzito mkubwa kutokana na ukweli wapinzani wao, KMC wameonekana kuimarika kwa siku za karibuni, hivyo hawataki kuharibiwa rekosi yao.

Yanga na KMC zinakutana kesho katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara, huku wenyeji wakichekelea ushindi wa 1-0 iliyopata kwenye mchezo wa awali mwaka jana.

Zahera aliyeiongoza Yanga katika mechi 26 kukusanya alama 64 ikiwa imepoteza mechi mbili, alisema hawataidharau KMC lakini dhamira yake ni kupata ushindi ili wazidi kujiimarisha kileleni. KMC ipo nafasi ya nne ikiwa na alama 41 baada ya kushuka uwanjani mara 28 licha ya kuwa ni msimu wao wa kwanza kucheza Ligi Kuu na inafundishwa na Kocha Etienne Ndayiragije ambaye amekuwa akitajwa kuwaniwa na Azam FC kwa sasa.

Mbali na mechi hiyo ya kesho, leo ligi hiyo itashuhudia mechi tatu zikichezwa, Mtibwa Sugar itakuwa Manungu, Morogoro kuikaribisha Stand United mapema mchana kabla ya jioni Kagera Sugar na Wagosi wa Kaya, Coastal Union kupepetana Kaitaba, mjini Bukoba huku Lipuli na Mbao FC zikiwa Uwanja wa Samora, mjini Iringa.

Kesho mbali na mechi ya Yanga na KMC, pia kutakuwa na mchezo mwingine mmoja utakaoanza mapema kati ya Mwadui dhidi ya Mbeya City itakayochezwa Mwadui Complex mjini Shinyanga.



Chanzo: mwananchi.co.tz