Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga kuivaa Mwadui leo

432c801f27a469f81c9634ce2fcabb86.jpeg Yanga kuivaa Mwadui leo

Sun, 20 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

YANGA leo itaikabili Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Benjamin, Mkapa, Dar es Salaam saa 1:00 usiku.

Yanga imetoka kushinda mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting kwa mabao 3-2 kwenye Uwanja huo na kuendelea kubaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 64.

Mwadui ambayo imeshashuka daraja, imetoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1 uliochezwa Shinyanga juzi.

Mchezo huo ni muhimu kwa Yanga kujiweka katika mbio za ubingwa na Mwadui licha ya kuwa imeshuka daraja ikiwa na pointi 19 sio timu ya kubezwa kwani imekuwa ikicheza kwa matumaini kutafuta matokeo mazuri.

Timu hizi zimekutana mara mbili na katika mchezo wa Ligi Kuu Yanga ilishinda mabao 5-0, ilikutana Shinyanga katika mchezo wa robo fainali wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) Yanga ikashinda kwa mabao 2-0.

Kwa tofauti hiyo, Mwadui inaweza kuonesha ushindani ingawa katika ubora kuanzia safu ya ushambuliaji na hata ulinzi bado Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri kulingana na watakavyojipanga.

Mchezo mwingine utakaochezwa leo ni Kagera Sugar dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera.

Kagera imetoka kushinda mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons bao 1-0 na kufufua matumaini ya kujiondoa katika nafasi za hatari, ingawa bado wanahitaji kushinda ili kujiweka pazuri zaidi kwani nafasi ya 12 waliyopo sio salama.

Hata Ihefu wanahitaji matokeo mazuri kutoka katika nafasi ya 15 na wakifungwa watakuwa hatarini zaidi.

Biashara itakuwa mwenyeji wa JKT Tanzania katika Uwanja wa Karume, Mara na wenyeji wanahitaji ushindi kuendelea kubaki nafasi ya nne.

Endapo watapoteza na walioko chini yao ambao wametofautiana kwa pointi kidogo wakishinda watakuwa kwenye presha ya kuondolewa.

Kwa upande wa JKT Tanzania ambao wako katika nafasi ya 14, wanahitaji kupambana kushinda mchezo huo ili kupanda juu zaidi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz