Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga imefeli ijipange kwa mabadiliko

Cd39727ecb4f228040def5709930d401 Yanga

Sat, 18 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MABINGWA wa kihistoria Yanga wamebaki katika historia, lakini si wale waliojulikana miaka kadhaa iliyopita kwa ubora na  sifa za kila aina

Katika miaka ya karibuni, Yanga walikuwa ni wagumu kuongozwa na wapinzani wao miaka mitatu mfululizo pasipo kufanya mapinduzi, lakini awamu hii wameshindwa kufurukuta. Ni zaidi ya miaka 16 iliyopita, timu hiyo yenye makao yake makuu mitaa ya Jangwani Kariakoo kuongozwa mara nne tena na mpinzani wake mkubwa alikuwa ni Simba.

Simba ilichukua taji la ligi mara nne mfululizo kuanzia mwaka 2001 hadi 2004 na baada ya hapo walikuwa wakipokezana na Yanga na baadaye Azam ikachukua mara moja. Kuanzia miaka hiyo, Yanga ilikuwa haimwachii nafasi Simba miaka miwili au mitatu, lazima wafanye mapinduzi na wakichukua basi ni miaka miwil au mmoja ndipo humwachia mpinzani wake.

Mara ya mwisho Yanga kuchukua mataji mara tatu mfululizo ni msimu wa 2014/2015, 2015/2016 na 2016/2017.

Huko nyuma walikuwa bora kusajili wachezaji wenye majina ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, walikuwa wanaogopeka kwa timu pinzani kwenye ligi na walikuwa washindani wakubwa wa watani zao wa jadi Simba.

Pia, hata mashabiki wao walikuwa wanajitokeza kwa wingi uwanjani wakijiamini kipindi ambacho walikuwa wakikutana na watani zao Simba tofauti na miaka hii ya karibuni wamekuwa ni watu wenye hofu.

Baada ya hapo unaweza kusema walikumbwa na upepo mbaya wakajikuta mwenendo wao ukiporomoka sio tu kwenye ligi hata Kombe la Shirikisho na michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

YANGA YA SASA

Imepoteza mataji: Ni msimu wa tatu inapoteza nafasi ya kushinda mataji na uwakilishi wa kimataifa. Msimu uliopita walishiriki baada ya Simba kuwakomboa kwani ilipotinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliongeza pointi zilizochangia kupata uwakilishi wa timu nne kwenye michuano hiyo ya kimataifa na yeye akiwa mshindi wa pili kwenye ligi alichaguliwa.

Lakini haitashiriki tena mwakani kitendo ambacho kinaweza kuishusha pia, kwenye viwango vya klabu bora Afrika vinavyotolewa kila mwaka.

IMEPOTEZA USHINDANI:

Yanga imekuwa ikikabiliwa na upinzani mkali sio kwa Simba ambao wameonekana bora kuwashinda, bali hata timu nyingine ndogo. Wamekuwa wakihangaika kupata matokeo mazuri. Sio ajabu wao kufungwa na timu ndogo.

Lakini ilikuwa ni ngumu Yanga kufungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani na timu ndogo. Msimu huu imetokea baada ya kuruhusu kutawaliwa na Ruvu, Kagera Sugar na wengine. Mfano Ruvu iliwafunga bao 1-0 na Kagera mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Uhuru,Dar es Salaam. Ukiachilia mbali watani zao wa jadi, ambao wamekuwa wakifungana kwa vipindi tofauti.

USAJILI MBOVU:

Timu hii imekosa watu wazuri wa kusaka vipaji na matokeo yake wamekuwa wakisajili wachezaji wengi wenye viwango vya chini kiasi cha kushindwa kuwasaidia. Msimu huu tu, ilisajili zaidi ya wachezaji 20 kisha ilipofika kwenye dirisha dogo waliachwa wengi wa kimataifa wakasajili wengine tena ambao kuna baadhi bado viwango vyao havikidhi.

Mara ya mwisho Yanga kuwa na wachezaji wengi wazuri ni pale walipochukua mataji matatu mfululizo na baada ya hapo wakapotea kutokana na baadhi ya wachezaji kuondoka, wengine kuachwa kutokana na umri na baadhi yao kuuzwa.

HAMASA IMEPOTE:

Wachezaji wengi wa Yanga wa zamani walikuwa wakicheza kwa kujitolea sana hata kama hamna pesa au kuna migogoro tofauti na miaka hii,  ambapo maslahi yako mbele zaidi kuliko kiwango uwanjani. Yanga ilikuwa ikisifiwa kuwapata wachezaji wenye mapenzi, wanaopenda timu na wanaopambana uwanjani. Leo wako wapi? Mambo yamebadilika kinachoangaliwa ni pesa mbele.

UKATA MKALI:

Tangu kuondoka kwa aliyekuwa mfadhili wao Yusuf Manji timu hiyo imekuwa ikipitia kipindi kigumu. Imekuwa ikipitisha bakuli kwa wanachama wake lakini bado fedha walizokuwa wakichangisha hazijawasaidia kwani uendeshaji umekuwa na gharama.

Kuna wakati utasikia wachezaji wamegoma hawajalipwa miezi miwili, mitatu na kuendelea. Wengine utasikia hawajalipwa ada ya usajili na mambo kadha wa kadha.

Lakini pia, huenda ukata umechangia kwa kiasi kikubwa timu kushindwa kusajili wachezaji wa viwango vya juu na badala yake mdhamini mmoja mmoja mpaka ajitolee kusaidia kwa kununua mchezaji au viongozi wenye pesa kununua wachezaji.

Hayo yanaweza kuwa ni mambo yaliyowafelisha na kushindwa kupata timu bora yenye ushindani. Suala hilo limedumu kwa muda kwa misimu hii mitatu mfululizo kiasi cha kuwafanya mmoja wa wadhamini wao GSM kuingilia kati na kuwasaidia baadhi ya mambo, ikiwemo kuwalipa mishahara wachezaji wachache, kutoa bonasi kwa timu kwa ajili ya hamasa la sivyo huenda mambo yangekuwa magumu zaidi kwao. Ni kweli wanajitahidi kwenye ligi kumaliza nafasi za juu lakini haiwasaidii kama hawachukui mataji na kuwakilisha kimataifa hivyo, wanahitaji kufanya kitu kurudi katika ubora wao.

UKAKASI MASHABIKI:

Mashabiki wao wamekuwa ni watu wanaoikatisha timu tamaa. Kwa mfano klabu hiyo iliwahi kuanzisha mfumo wa wanachama kuchangia kuanzia Sh 1000 na baadhi walionyesha mwitikio lakini jambo la ajabu kadiri siku zilivyokwenda walipunguza kuchanga.

Kingine, mashabiki wa Yanga wamekuwa hawajitokezi kwa wingi uwanjani kuunga mkono timu yao hasa inapokuwa nyumbani. Kama wangekuwa wanajitokeza na kujaza uwanja labda wangekuwa wanasaidia kupunguza sehemu ya mzigo kwenye klabu hiyo. Matokeo yake wamekuwa ni watu wa kulaumu hasa pale timu yao inapopata matokeo mabaya.

SULUHISHO KUBWA :

Wanachotakiwa kufanya ni kuendelea kushirikiana na wadhamini wao ikiwemo GSM ambao wameonesha nia ya dhati ya kuwasaidia kuingia kwenye mchakato wa mabadiliko.

GSM imewaahidi mambo mengi, kwanza ni kusajili kikosi kizuri chenye ushindani msimu ujao. Ili hayo yaweze kutimia ni lazima waungane katika mchakato wa mabadiliko yaweze kutimia.

Wajifunze kwa watani zao wa jadi Simba ambao tangu kumruhusu mwekezaji Mohamed Dewji kununua hisa 49 ndani ya klabu hiyo timu imekuwa imekuwa katika mwenendo mzuri na wamekuwa wakijivunia mafanikio.

Ubora wa Simba hii leo haufanani na Yanga hata kidogo, wanahitaji kubadilika kuendana sawa katika ubora na ushindani ili hatimaye msimu ujao mambo yaweze kuwa mazuri zaidi kwao.

Muda wa wa Yanga kujipanga ni sasa wanachotakiwa kufanya ni kukamilisha mipango yao ya mabadiliko na kujipanga upya kwa msimu ujao, wakianzia na usajili mzuri.

 

 

Chanzo: habarileo.co.tz