Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga Yamuandalia Mkataba Kagere

Kagere Data Yanga Yamuandalia Mkataba Kagere

Fri, 30 Jul 2021 Chanzo: globalpublishers.co.tz

Yanga Yamuandalia Mkataba Kagere July 29, 2021 by Global Publishers



TAARIFA zilizopo ni kwamba, mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere, amewasilisha barua kwa uongozi wa klabu hiyo ya kuomba kusitisha mkataba wake ili kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine, huku ikielezwa kwamba muda wowote huenda akajiunga na Yanga ambayo imekuwa ikimnyemelea.

Kagere alikuwa na wakati mgumu kupata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba msimu wa 2020/21 uliomalizika hivi karibuni, kutokana na ushindani mkubwa wa namba kwenye safu ya ushambuliaji.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimelitonya Spoti Xtra kuwa, juzi Jumanne Kagere alikutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji ili kufikia makubaliano ya pande zote mbili kusitisha mkataba wake.

“Ni kweli Kagere amekutana na bosi MO, kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kufikia makubaliano ya pande zote mbili na kuachana na Simba, hii ni kutokana na mchezaji huyo kuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu kuzungumzia suala hilo, alisema: “Kwangu binafsi nisingependa kuliongelea suala ambalo bado halijafanyiwa uamuzi na Bodi ya Wakurugenzi, subiri mpaka tutakapokaa na kufikia uamuzi, tutatoa taarifa.”

Wakati hayo yakijiri, upande wa Yanga kumekuwa na shangwe kubwa ambapo mashabiki wa timu hiyo wanasubiri muda ufike tu Mnyarwanda huyo atambulishwe kikosini kwao.

Yanga wamepata matumaini hayo baada ya hivi karibuni, mmoja Kati ya viongozi ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliliambia Spoti Xtra kuwa: “Msimu huu lazima tutawashangaza watu kwa kusajili mchezaji mkubwa kutoka katika moja ya klabu kubwa Tanzania.

Muda ukifika mtaona.”Kauli hiyo inaashiria huenda akawa ni Kagere ambaye ndani ya Simba, amekuwa mchezaji mwenye jina kubwa kutokana na kufanya makubwa kwa misimu miwili ya kwanza akiibuka mfungaji bora mfululizo.

Kwa muda wa misimu mitatu ambayo Kagere ameichezea Simba kwenye Ligi Kuu Bara pekee, amefanikiwa kufunga mabao 58, ambapo msimu wa 2018/19 alifunga mabao 23, 2019/20 mabao 22 na 2020/21 mabao 13.

Mnyarwanda huyo alijiunga na Simba mwaka 2018 akitokea Gor Mahia ya Kenya, huku hivi karibuni ikiripotiwa kwamba aliongeza mkataba wa kuendelea kuichezea Simba hadi 2023.

STORI: WAANDISHI WETU

Share this:TweetWhatsApp Related

Chanzo: globalpublishers.co.tz