Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Simba, Gor Mahia, KCCA zakalia kuti kavu

71476 Cecafa+pichha

Thu, 15 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Timu za ukanda wa Afrika Mashariki zinakabiliwa na presha kubwa ya kutumia vyema kipindi cha wiki moja, kufanya maandalizi imara yatakayozifanya zisonge mbele kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu huu.

Klabu hizo 12 kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Tanzania na Zanzibar zimejiweka katika kibarua kigumu cha kuhakikisha zinapindua matokeo ya mechi za kwanza ili kusonga mbele vinginevyo zitajikuta zikiaga mashindano hayo mapema.

Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Afrika Mashariki inawakilishwa na timu za Gor Mahia ya Kenya, Aigle Noir (Burundi), Rayon Sports (Rwanda), KCCA (Uganda), KMKM (Zanzibar) pamoja na Simba na Yanga zinazoiwakilisha Tanzania Bara.

Wawakilishi wa Afrika Mashariki kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ni Azam FC na KMC zinazopeperusha bendera ya Tanzania Bara, Malindi (Zanzibar), Bandari (Kenya), Rukinzo (Burundi), AS Kigali (Rwanda) na Proline (Uganda).

Matokeo ya mechi za kwanza za hatua ya awali ambazo timu hizo zilicheza kwenye viwanja vya ugenini na nyingine zikicheza nyumbani, yanauweka ukanda wa Afrika Mashariki kwenye hofu ya kuingiza timu chache kwenye hatua ya kwanza na pia ile ya makundi ambayo ndio lengo kuu kwa idadi kubwa ya klabu shiriki.

Katika kundi hilo la timu 12 kutoka Afrika Mashariki zinazoshiriki mashindano ya klabu Afrika, ni Proline FC ya Uganda ambayo imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu hatua inayofuata kutokana na ushindi wa mabao 3-0 ilioupata kwenye mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Masters Security ya Malawi.

Pia Soma

Proline ndio timu pekee iliyopata ushindi kwa timu kutoka ukanda huu kwenye mechi za kwanza na sare au ushindi wowote ugenini utawapeleka hatua inayofuata ambayo pia wanaweza kuingia hata wakipoteza kwa kichapo cha mabao 2-0 au 1-0.

Hali ni tete zaidi kwa timu za KMKM na Rukinzo ambazo zinategemea miujiza ili ziweze kupenya kwenye hatua inayofuata baada ya kupokea vichapo vizito kwenye mechi za kwanza.

KMKM ilichapwa kwa mabao 2-0 nyumbani na 1ยบ de Agosto ya Angola na inatakiwa ikaibuke na ushindi wa kuanzia mabao 3-0 ugenini wakati Rukinzo yenyewe ilichapwa mabao 5-0 ugenini dhidi ya Triangle United ya Zimbabwe na inatakiwa kuibuka na ushindi wa kuanzia mabao 6-0 nyumbani ili isonge mbele, jambo linaloonekana linaweza kuwa gumu kutokea.

Ukiondoa hao, Yanga, Rayon Sports, Aigle Noir na Bandari, zenyewe zinakabiliwa na kibarua kizito cha kuhakikisha zinapata ushindi kwenye mechi za ugenini ili zisonge mbele baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye mechi za nyumbani.

Bandari ilitoka sare ya bila kufungana na Al-Ahly Shendi, Rayon ikatoka sare ya bao na Al Hilal kama ilivyokuwa kwa Yanga na Township Rollers wakati Aigle Noir ilitoka sare ya bila kufungana na Gor Mahia.

Lakini pamoja na kutopata matokeo ya kuvutia kwenye mechi za kwanza timu za KCCA, Simba, Azam, KMC, Malindi na Gor Mahia zina nafasi kubwa ya kusonga mbele ikiwa zitatumia vyema fursa ya kumalizia mechi za hatua ya awali kwenye viwanja vya nyumbani.

Simba, KMC, Gor Mahia na Malindi kila moja ilitoka sare ya 0-0 ugenini na ushindi wowote nyumbani utawavusha, KCCA ilichapwa mabao 3-2 na African Stars ya Namibia hivyo inahitajika kupata ushindi wa bao 1-0 tu ili isonge mbele.

Kwa upande wa Azam FC yenyewe nayo inamlima mrefu kidogo kupanda kwani inatakiwa kuibuka na ushindi wa kuanzia mabao 2-0 nyumbani ili isonge mbele baada ya kuchapwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia.

Hata hivyo kitendo cha timu nne za Afrika Mashariki kukutana zenyewe kwa zenyewe kwenye hatua ya awali, kunaupa uhakika wa moja kwa moja ukanda huu kuwa na timu mbili kwenye hatua inayofuata kwa kuanzia.

Timu hizo mbili zitakuwa ni mshindi wa jumla baina ya Gor Mahia ya Kenya na Aigle Noir ya Burundi kama ilivyo kwa KMC ya Tanzania Bara na AS Kigali ya Rwanda

Kocha wa Azam FC, Etienne Ndayiragije alisema kuwa bado wana nafasi ya kusonge mbele na kutinga hatua inayofuata.

"Nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano ambayo tutakuwa nyumbani ipo na naamini Mungu akipenda tutafanya vizuri," alizungumza kwa kifupi Ndayiragije.

Chanzo: mwananchi.co.tz