Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga SC yatibua hesabu za Simba

28887 Yanga+pic TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kagera. Ushindi wa pili mfululizo katika mechi za ugenini, umeifanya Yanga kutibua hesabu za Simba na Azam katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Baada ya kupata matokeo mazuri katika mechi 10 mfululizo ilizocheza Dar es Salaam, matumaini makubwa ya Simba na Azam bila shaka yalikuwa ni kuikamata Yanga itakapoanza kucheza viwanja vya mikoani.

Kiwango duni ambacho Yanga ilikuwa ikionyesha katika mechi ilizocheza Dar e Salaam licha ya kupata ushindi, kilileta matumaini kwamba huenda timu hiyo ikakutana na upinzani mkali na kuangusha pointi itakapokwenda kucheza mechi za nje ya jiji.

Hata hivyo, ndoto hizo za wapinzani wa Yanga ni kama zimeyeyuka kwani mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamefanikiwa kukusanya pointi sita katika mechi mbili mfululizo walizocheza Kanda ya Ziwa.

Yanga ilianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga na kipigo cha mabao 2-1 walichoipa Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba hapa Kagera jana, kilitosha kuwafanya warudi Dar es Salaam wakiwa kifua mbele.

Dalili za Yanga kuibuka na ushindi katika mchezo wa jana zilianza kuonekana mapema baada ya kipyenga cha kuanza mpira huo kupulizwa kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara iliyokuwa ikipeleka langoni mwa Kagera Sugar.

Ikifanya mabadiliko kadhaa, Yanga ilionyesha kiu ya kusaka ushindi wa ugenini kwa kuanza kuishambulia Kagera Sugar ambayo ilionekana kuwasoma taratibu wapinzani wao huku ikishambulia kwa kushtukiza.

Katika mchezo huo benchi la ufundi la Yanga lilifanya mabadiliko mawili kwenye kikosi chake kilichoibuka na ushindi dhidi ya Mwadui kwa kuwaanzisha Haji Mwinyi na Ramadhani Kabwili waliochukua nafasi za Gadiel Michael na Klaus Kindoki.

Njaa ya Yanga kusaka ushindi ilizaa matunda mapema dakika ya 21 baada ya kupata bao la utangulizi kupitia kwa Heritier Makambo aliyeunganisha vyema kwa kichwa mpira wa krosi uliochongwa kutoka upande wa kushoto na Mwinyi.

Bao hilo lilitokana na shambulizi la haraka ambalo Yanga ililifanya ikijibu lile lililofanywa na Kagera Sugar ambao walikosa bao kupitia kwa Peter Mwalyanzi ambaye shuti lake lilipaa langoni.

Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuwaamsha Kagera Sugar ambao walianza kufunguka na kushambuliana kwa zamu na Yanga. Kagera Sugar ilipata bao la kusawazisha kupitia kwa Ramadhani Kapera aliyefunga kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika ya 31.

Penalti hiyo ilitokana na juhudi binafsi za Kapera ambaye aliwachambua mabeki wawili wa Yanga na kuingia kwenye eneo la hatari ambapo aliangushwa na kipa Kabwili ndipo mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara alipoamuru pigo la penalti.

Ndani ya dakika 10 za kipindi cha pili, Yanga ilifanya mabadiliko mawili ya haraka kwa kuwatoa Makambo na kumuingiza Ibrahim Ajibu, ilimtoa Mwinyi na kuingia Deus Kaseke. Dakika 11 baadaye ilimuingiza Rafael Daud badala ya Maka Edward.

Mabadiliko hayo yaliibeba Yanga baada ya Daud kufunga bao la pili dakika ya 75 kwa kichwa akiunganisha vyema mpira ulioanza kupigwa kichwa na Kaseke ambao ulitokana na krosi ya beki Paul Godfrey.

Yanga imefikisha pointi 32 ikiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya Azam inayoongoza huku ikiwa na pointi tano zaidi ya Simba inayoshika nafasi ya tatu.

“Naomba nitoe ujumbe kwa TFF waangalie mwenendo wa Ligi. Timu zinatumia nguvu na gharama kubwa lakini waamuzi wanaharibu,” alisema Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera.

“Tumefanya makosa mawili yametugharimu, lakini pia tumepambana tumeshindwa kupata matokeo,” Kocha Mkuu wa Kagera Sugar,Mecky Maxime.

Wakati huohuo, timu ya Taifa ya soka la ufukweni (Beach Soccer) imetwaa ubingwa wa mashindano maalumu ya kirafiki ya Copa Dar es Salaam. Timu hiyo iliichapa Uganda mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jana ufukwe wa Coco Beach jana.

Ushindi huo ambao umeipa ubingwa Tanzania jana, ni muendelezo wa matokeo bora ambayo imekuwa ikiyapata kwenye mashindano hayo kwani kabla ya hapo iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Malawi, iliichapa Uganda mabao 10-2 na pia iliibuka na ushindi wa mabao 7-4 dhidi ya Shelisheli kwenye hatua ya makundi.



Chanzo: mwananchi.co.tz