Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga SC yaichapa Stand, mashabiki wake wanuna

17807 Pic+yanga TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya Yanga kuendelea kuionea Stand United ‘Chama la Wana’ ya Shinyanga, katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, timu hiyo bado haijapata ufumbuzi wa tatizo la kipa.

Yanga jana ilishuka kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuikaribisha Stand na ilijipatia mabao ya haraka haraka ikienda mapumziko kifua mbele ikiongoza kwa mabao 3-1.

Hata hivyo, makosa yaliyofanywa na kipa wake mpya Klaus Kindoki raia wa DR Congo yalimuwezesha Alex Kitenge kufunga mabao matatu ‘hat trick’ ya kwanza katika Ligi ya msimu huu licha ya timu yake Stand kulala kwa mabao 4-3 jambo lililowakera mashabiki wake.

Kabla ya msimu kuanza, Yanga ilimtupia virago kipa raia wa Cameroon, Youthe Rostand kutokana na kufanya makosa mengi akiwa langoni yaliyoigharimu timu na kumsajili Kindoki, lakini naye jana alionyesha udhaifu ambao nusura uigharimu timu hiyo.

Katika mchezo wa jana, Yanga ilianza kujipatia bao la kuongoza katika dakika ya pili ya mchezo likifungwa na Mrisho Ngasa, aliyewazidi ujanja mabeki wa Stand akiuwahi mpira mrefu aliopasiwa na Ibrahim Ajib.

Ajib aliongeza bao la pili katika dakika ya 32 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya Pappy Tshishimbi na kupiga shuti kali akimuacha kipa Mohammed Makaka asijue la kufanya.

Dakika tatu baadaye, Yanga ilijipatia bao la tatu lililofungwa na mlinzi Andrew Vicent ‘Dante’ aliyepanda mbele kuongeza nguvu baada ya Yanga akiunganisha kwa kisigino mpira wa adhabu uliopigwa na Ajib. Alifunga akitumia vyema makosa ya kipa wa Stand aliyetoka vibaya langoni. Kitenge ambaye licha ya kipigo hicho aliibuka shujaa, alianza kuifungia Stand bao la kwanza dakika ya 42.

Yanga ilianza kipindi cha pili kwa nguvu na kufanikiwa kujipatia bao la nne katika dakika ya 57 lililofungwa na Deus Kaseke akiitendea haki pasi ya Ajib, ambaye jana aling’ara kwani licha ya kufunga, alitoa pasi za mabao matatu.

Kitenge alifunga mabao mengine mawili katika dakika za 59 na 90 yaliyowafanya mashabiki wa Yanga kuingiwa na wasiwasi wakati wote wa dakika nne za nyongeza, kwani ilionekana kama Stand ingesawazisha dakika yoyote kutokana na kufanya mashambulizi mfululizo.

Hata hivyo, hadi mwamuzi Benedict Magai kutoka Mbeya anapuliza kipenga cha mwisho, Yanga ilitoka uwanjani na pointi zote tatu ikijipatia ushindi wa pili katika mechi mbili za ligi hiyo ilizocheza hadi sasa ikiwa na kiporo cha michezo miwili.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Yanga imeendelea kuitambia Stand kwa kushinda kila zinapokutana kwenye uwanja wa Taifa. Kabla ya ushindi wa jana, zilianza kukutana April 21, 2015 na Yanga kushinda 3-2 na mara ya mwisho iliichapa 3-1 Machi 3 mwaka huu.

Kikosi kilichoanza Yanga jana ni, Klaus Kindoki, Paul Nyanganya, Gadiel Michael, Andrew Vicent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mrisho Ngasa, Papy Tshishimbi, Heritier Makambo, Ibrahim Ajib na Deus Kaseke.

Chanzo: mwananchi.co.tz