Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga SC yaanika ukweli kipigo cha Gor Mahia

9539 Pic+yanga TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, kudai Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limechangia kipigo chao dhidi ya Gor Mahia, wachezaji wa timu hiyo wameanika ukweli namna walivyoathirika na tukio la kuondolewa kambini saa chache kabla ya mchezo.

Mwandila aliyekuwa kwenye benchi katika mchezo wa Kombe la Shirisho Afrika, alidai kitendo cha TFF kuwachukua kambini wachezaji wake kilichangia Yanga kupoteza mchezo huo.

Katika mchezo huo, Yanga ilifungwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufuta ndoto ya kufuzu robo fainali ya mashindano hayo mwaka huu.

Wakizungumza Dar es Salaam jana ,baadhi ya wachezaji wa Yanga waliochukuliwa kwenda kupiga picha za matangazo ya udhamini wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ wameeleza athari iliyowapata muda mfupi kabla ya kuivaa Gor Mahia.

Beki tegemeo Andrew Vincent ‘Dante’ alisema tukio la kupiga picha za matangazo lilichangia kwa kiasi kikubwa kuwaathiri.

“Tulipigiwa simu siku hiyo tukaombwa twende Uwanja wa Taifa kupiga picha, tuliambiwa zoezi litaanza saa nane mchana tulitegemea hadi saa 10 tutakuwa tumemaliza, lakini hali ilikuwa tofauti na matarajio yetu,” alisema Dante.

Beki huyo wa kati alisema hawakufuatwa na kiongozi yeyote wa TFF waliondoka wenyewe kwenda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kupata maelekezo.

“Hatukutarajia kama tukio hilo lingefanyika hadi usiku sana kwa kweli lilitusababishia uchovu kwa sababu hatukutarajia lingechukua muda mrefu kiasi kile,” alisema Dante.

Naye mshambuliaji Deus Kaseke alisema waliondoka kambini saa nane mchana kwenda kupiga picha na walirejea kambini saa sita usiku ingawa walikua wakikabiliwa na mchezo dhidi ya Gor Mahia, jioni ya siku iliyofuata.

Kaseke aliyefunga moja ya mabao katika mchezo huo, alisema upigaji wa picha ulikuwa wa aina tofauti, zikiwemo za kushangilia.

Anasema katika tukio la upigaji picha walikuwepo wachezaji wa Yanga pekee hatua aliyodai ilichangia kupata uchovu kutokana na idadi yao kuwa ndogo.

Wachezaji wengine waliochukuliwa kwenda kupiga picha ni Ramadhani Kabwili, Ibrahim Ajibu, Raphael Daudi na Gadiel Michael.

Tukio la wachezaji wa Yanga kupigwa picha muda mfupi kabla ya mchezo, limewaibua wachambuzi wa soka nchini ambao walidai klabu hiyo haikutendewa haki hata kidogo na TFF.

“Mchezaji anahitaji muda mrefu wa kupumzika hasa akiwa anajiandaa na mechi, lakini kwa hili la Yanga inaweza limewaathiri ingawa sio moja kwa moja,” alisema Ally Mayay.

Alisema mchezaji asiyekuwa fiti lazima imuathiri na ndicho kilichotokea Yanga kwa kuwa wachezaji wake walionekana kutokuwa na utimamu wa mwili.

“Pasi zilizokuwa zinapotea kwenye mchezo huo ni moja ya kipimo kuwa utimamu wa mwili kwa timu yote haukuwepo, mfano mchezaji pasi mbili anapoteza moja maana yake nusu ya pasi zilipotea, hivyo kutokuwa fiti na kuchangia kutopata muda wa kupumzika kumechangia matokeo hayo,” alisema Mayay.

Mchambuzi mwingine, Joseph Kanakamfumu alisema siku moja kabla ya mechi mchezaji anahitaji kupata muda mrefu wa kupumzika ili kutunza nguvu kwa mchezo unaomkabili.

“Baada ya mazoezi anatakiwa alale na kama asipolala basi apate tu muda wa kupumzika, kazi yake iwe kula na kurudi kupumzika ili kuhifadhi nguvu,” alisema Kanakamfumu.

Akizungumza tukio hilo, Rais wa TFF Wallace Karia alidai Yanga haipaswi kulalamika kuwa tukio la upigaji picha haliwezi kuwa sababu ya kupoteza mchezo huo.

“Mbona walifungwa mabao 4-0 Kenya, waache malalamiko ,” alisema Karia kwa kifupi.

Chanzo: mwananchi.co.tz