Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga SC kuikwepa mbeleko Simba CAF

Yangaaaa Ed Yanga SC kuikwepa mbeleko Simba CAF

Tue, 6 Apr 2021 Chanzo: ippmedia.com

Kitendo cha Simba kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kimeiongezea Tanzania pointi na sasa ipo katika nafasi ya kuingiza timu nne kwenye michuano ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF); timu mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho.

Bingwa wa Ligi Kuu Bara, hukata tiketi ya moja kwa moja kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika huku mshindi wa Kombe la FA, akikata tiketi ya Kombe la Shirikisho na timu inayoshika nafasi ya pili na tatu ndizo hupewa dhamana ya michuano ya kimataifa endapo Tanzania ikiwa na tiketi ya kuingiza timu nne.

Lakini Ofisa Habari wa Yanga, Hasan Bumbuli, amesema kuwa nia yao msimu huu ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa tiketi yao wenyewe na si ya kukatiwa na timu nyingine.

Bumbuli alisema hayo alipoulizwa juu ya ushindi wa Simba wa mabao 4-1 dhidi ya AS Vita ilioupata Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao umeiweka Tanzania kwenye mazingira mazuri ya kuongeza timu msimu ujao kwenye michuano ya kimataifa.

"Mimi sijasikia matokeo yoyote ya Simba. Ila kama wameshinda basi sawa, lakini kusema eti watatubeba kwenye mechi za kimataifa, labda wawabebe wengine siyo sisi. Yanga tutakwenda kwa nguvu zetu wenyewe kwenye michuano ya kimataifa kwa sababu kwa sasa tunaongoza ligi na tunausaka ubingwa, nina imani tutaupata na hatutohitaji kutafutiwa nafasi na mtu," alisema Bumbuli wakati huu timu yao ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu na pointi 50 ikifuatiwa na Simba yenye alama 46, lakini ikiwa nyuma kwa michezo mitatu.

Chanzo: ippmedia.com