Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Biashara hesabu tupu

90349 Yanga+pic Yanga, Biashara hesabu tupu

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaendelea leo na jumla ya viwanja vitano vitawaka moto lakini mchezo mkubwa utakuwa pale Uwanja wa Uhuru ambapo Yanga itaikaribisha Biashara ya Mara katika mchezo wa hesabu.

Yanga ambayo inarudi nyumbani ikitokea Mkoani Mbeya ambapo ilikwenda kutafuta pointi sita na kuambulia nne dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons inakutana na Biashara katika mchezo wa mtego.

Mtego ni kwamba Yanga baada ya mechi hii itakuwa na homa nzito ya kukutana na watani wao Simba mchezo utakaopigwa Januari 4, itahitaji ushindi kujihakikishia morali nzuri kwa kikosi chao na hata mashabiki wao kabla ya wekundu hao nao kushuka uwanjani kesho kupambana na Ndanda ya Mtwara inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani.

Yanga inatambua ugumu wa mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza ugenini dhidi ya Biashara msimu uliopita lakini hata ule wa kwanza ilishinda kwa mbinde dakika za majeruhi mabao 3-2.

Jeuri pekee kwa Yanga ni kwamba inatoka kuichapa Prisons ambayo tangu ligi ianze ilikuwa haijafungwa na hata Simba ilishindwa kuifunga ikiwa nyumbani hiyo ndiyo jeuri pekee itakayoisukuma kusaka pointi tatu za mchezo huo.

Yanga ambayo iko katika nafasi ya tatu inaona hapo si sehemu yenye hadhi yao ikiwa na pointi 21 juu yao ipo Kagera Sugar yenye pointi 24, ushindi wao katika mchezo wa leo utaifanya kuzidi kusogelea nafasi mbili za juu.

Nahodha wa Yanga Pappy Tshishimbi alisema wanatambua ugumu wa mchezo huo lakini wana kiu kubwa na pointi tatu za mechi hiyo.

“Mchezo huu tunacheza na Biashara lakini tunahitaji pointi tatu kwa malengo ya mchezo unaokuja dhidi ya Simba, matokeo mazuri ya mchezo wa kesho (leo) yatatupa morali zaidi katika kujiandaa na kukutana na Simba,”alisema Tshishimbi.

“Nimekuwa nikiwaambia wenzangu juu ya utulivu katika mchezo huu hii ni klabu kubwa lazima ipate morali nzuri inapokwenda kukutana na Simba, tumejiandaa vizuri hasa baada ya kupata pointi nne kule Mbeya.

“Tutakuwa nyumbani mbele ya mashabiki wetu tunaamini mchezo utakuwa mgumu lakini ushindi mzuri ndio dhamira yetu kubwa, kama unavyoona muda unavyokwenda tunazidi kuongeza ubora katika kikosi chetu.”

Wakati Yanga ikijipanga Biashara ambayo iko Dar es Salaam tangu juzi, imetamba kwamba wanazidi kukaa vizuri tangu ujio wa kocha mpya Mkenya Francis Baraza.

Baraza anakutana na Yanga ukiwa ni mchezo wake wa kwanza na wakongwe hao lakini pia anacheza mechi ya kwanza nje ya mkoa wao wa Mara ambapo alisema anaiheshimu Yanga.

Tumekuwa katika ubora mzuri nimekuwa nikibadilisha baadhi ya mifumo hapa karibu kila mchezo naona ina tija tunakwenda kukutana na Yanga ambayo ni wakongwe na timu kubwa tunawaheshimu lakini hatuwaogopi,”alisema Baraza.

“Vijana wangu wako sawa tumejiandaa vizuri naamini wanatambua umuhimu wa ushindi katika mechi dhidi ya Yanga utaongeza kitu kwao kama wakipambana vizuri mwisho natambua hautakuwa mchezo rahisi itatulazimu kupambana, nimewaangalia Yanga katika mechi tatu kwa luninga ni timu ambayo inafunga pia inaweza kufungwa,” alisema Baraza.

Mchezo mwingine utakuwa pale Mabatini Mlandizi Ruvu Shooting dhidi ya Kagera Sugar ambao utakuwa ni vita ya mwalimu na mwanafunzi.

Ruvu inayofundishwa na kocha Salum Mayanga anakutana na mwanafunzi wake Mecky Maxime ambapo mara ya mwisho walipokutana kila mmoja aliambulia pointi tatu kwa mwenzake wakati huo Mayanga akiwa Mtibwa Sugar.

Mkoani Tanga Coastal Union iliyochini ya kocha Juma Mgunda yenye morali nzuri baada ya kuwachapa Azam watawakaribisha Mbeya City inayofundishwa na Amri Said.

Mtibwa Sugar itavaana na Alliance ya Mwanza na kocha wa Zuberi Katwila alisema:”Tuko tayari kwa mchezo.

Lipuli inarejea nyumbani baada ya kupoteza kwa mabao 4-0 dhidi ya Simba itaikaribisha Mbao ya Mwanza kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Chanzo: mwananchi.co.tz