Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yametimia Manji ajiengua Yanga

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanachama na mashabiki wa Yanga sasa wanapaswa kujiandaa kisaikolojia kuishi maisha bila Yusuf Manji baada ya jina la mwenyekiti huyo kutokuwapo miongoni mwa wagombea 27 waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa klabu hiyo utakaofanyika Janauri 13, 2019.

Tofauti na ilivyotarajiwa Manji hajachukua wala kuchukuliwa fomu kama ambavyo kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilitaka Yanga wafanye endapo watahitaji kumrejesha mwenyekiti huyo, badala yake wanachama wanne wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Mwanasheria wa TFF, Herman Kidifu aliwataja wagombea waliojitosa kuwania nafasi ya Mwenyekiti ni Dk Jonas Tiboroha, Yono Kevela, Mbaraka Igangula na Erick Ninga.

Wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti ni Titus Osoro, Salum Magege Chota na Kevela wakati wajumbe ni Hamad Ally Islamu, Benjamin Jackson Mwakasonda, Sylvester Haule, Salim Seif, Musa Katabaro, Shftu Amri na Said Baraka.

Wengine ni Pindu Luhoyo, Dominick Francis, Seko Jihadhari, Ally Omary Msigwa, Arafat Ally Haji, Geofrey Boniphace Mwita, Frank Kalokola, Ramadhan Said, Leonard Marango, Bernard Faustin Mabula, Christopha Kashiririka, Athanas Peter Kazige na Faustin Peter Bisangwa.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Ally Mchungahela alisema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu umefungwa rasmi na keshokutwa Ijumaa utafanyika mchujo kwa wagombea wote.

“Uchaguzi uko palepale kwa wagombea waliochukua fomu, baada ya mchujo wa Ijumaa kutakuwa na usaili na baadaye wagombea wataingia kwenye kampeni kuelekea katika uchaguzi,” alisema Mchungahela.

Mchungahela alitoa onyo kwa mtu yeyote atakayejaribu kujipenyeza kuvuruga mchakato wa uchaguzi kwa kuanzisha vurugu, kuwa vyombo vya dola vitafanya kazi yake.

Wakati Yanga ikitarajiwa kupata viongozi wapya, baadhi ya wadau wamewashauri wanachama wa klabu hiyo kubadili fikra ya kumtegemea mtu, badala yake waamini mfumo bora ndiyo utawafikisha kwenye mafanikio wanayohitaji.

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Ally Mayay alisema Yanga inatakiwa kukubali mabadiliko kwa kuwa hayakwepeki ingawa upo wasiwasi kutokana na maisha ya Yanga wakati wa Manji.

“Yanga hawana namna inabidi wakubaliane na hali halisi huu ni wakati wa kutegemea mfumo na siyo kumtegemea mtu, ‘solution’ kwao ni kuwa na mfumo ambao hata Manji asipokuwepo utaiweka klabu katika mazingira salama,” alisema Mayay.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Kanali Mstaafu, Idd Kipingu alisema kiongozi atakayechaguliwa anapaswa kuwa na uwezo wa kuiwzesha klabu inakuwa na vyanzo vingi vya mapato, lakini siyo kutegemea fedha kutoka mfukoni kwa mtu.

“Dunia ya sasa kila kitu kinaeleweka, hakuna asiyefahamu timu kama Barcelona, Real Madrid na nyinginezo za wananchi zinaongozwaje, bahati nzuri hapa nchini, Simba imeanza ni wazi hata bila Manji kama Yanga wakiamua watafika kwenye mafanikio wanayohitaji,” alisema Kipingu.

Aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi alisema ni wakati wa Wanayanga kujiandaa na kuruhusu kupokea mabadiliko.

Mkemi, alisema viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo akiwamo mwenyekiti mpya wahakikishe wanafuata Katiba ya klabu inavyohitaji.

“Katiba ya Yanga iko wazi, klabu inapaswa kujiendesha kibiashara, kilichopo ni utekelezaji, tuondokane na fikra ya kumtegemea mtu, hatuhitaji wala kubadili Katiba yetu ili twende kwenye mabadiliko ya uendeshaji, twende kwenye uchaguzi, watakaochaguliwa waanze mchakato klabu ijiendeshe kibiashara,” alisema Mkemi.



Chanzo: mwananchi.co.tz