Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yaliyojiri Yanga, Ruvu Shooting ndiyo tunayataka Ligi Kuu Bara

73549 Yanga+ruvu+pic

Fri, 30 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

JUZI Yanga walikumbana na kipigo kisichotarajiwa baada ya kulala 1-0 dhidi ya timu ambayo wamekuwa wakiinyanyasa kwa miaka mingi, Ruvu Shooting.

Katika mechi 18 zilizokuwa zimetangulia kabla ya juzi, Yanga ilikuwa imeifunga Shooting mara 15 na tatu zilizosalia walikuwa wametoka sare. Yaani Shooting walikuwa hawajashinda hata mechi moja kati ya hizo.

Lakini juzi katika hali isiyotarajiwa, Yanga ilikumbana na kipigo cha bao moja la dakika ya 20 lililodumu hadi mwisho wa mchezo.

Yanga waliingia katika mechi ya juzi kwa kishindo, huku hali ya kujiamini ikiwa juu kabisa.

Walikuwa wakicheza mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu ya Bara wakiwa na kikosi kipya kilichosajiliwa kwa pesa ndefu.

Na zaidi walikuwa ndiyo kwanza wametokea kushinda mechi yao ya Ligi ya Mabingwa ugenini Botswana walikowatoa Township Rollers ya huko kwa bao 1-0.

Pia Soma

Advertisement   ?

Wachezaji walipokewa kwa mbwembwe walipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere saa saba za usiku, hivyo mzuka wa mechi ulikuwa juu kabisa Jangwani.

Ndiyo sababu kipigo kutoka kwa timu ambayo wamekuwa wakiinyanyasa kwa miaka yote hakikuwajia kabisa katika fikra zao.

Lakini soka sio historia ama rekodi, bali ni dakika 90 zinazochezwa siku husika na ndiyo maana Shooting wakawashangaza Yanga kwa kipigo.

Yanga wanaweza kujitetea kwamba kipigo hicho kimechangiwa na kikosi chao kujaza wageni ambao watahitaji muda hadi kuzoeana na kutengeneza timu ya ushindani, lakini bado ni lazima wajiulize ilikuwaje wakafungwa na timu ndogo wanayoinyanyasa kila mwaka.

Na wakati Yanga wakijiuliza, wapenda maendeleo wote wanapaswa kujivunia matokeo yale kwenye Uwanja wa Uhuru.

Wanapaswa kuutazama ushindani ulioonyeshwa na Shooting katika mechi ile kwa jicho matumaini.

Matumaini kwamba tunaelekea kwenye Ligi Kuu yenye matokeo yasiyotabirika.

Ushindani unaotoa matokeo yasiyotabirika ni kati ya vitu vinavyoongeza mashabiki viwanjani na hiyo ni ishara ya kukua kwa soka la nchi.

Kiwango cha soka la nchi kinategemea, pamoja na mambo mengine, wachezaji wanaocheza soka la ushindani.

Tanzania kwa kuwa haina wachezaji wengi wanaocheza kwenye ligi zenye ushindani nje ya nchi, basi ni jambo la muhimu sana kuwa na ligi ya nyumbani yenye ushindani.

Lakini kwa bahati mbaya ni kwamba kwa miaka mingi, ligi ya nyumbani imekuwa ikiandamwa na tuhuma za wachezaji, makocha na hata waamuzi kuhusika katika upangaji wa matokeo.

Kwamba si mechi zote zinazochezwa na kutoa matokeo halali ya uwanjani.

Imekuwa ikidaiwa kwamba mechi nyingi huamualiwa nje ya uwanja.

Waamuzi wameshaingia matatani kwa tuhuma za kupokea rushwa, viongozi wa klabu wameshatuhumiwa kuhonga waamuzi ili wazipendelee timu zao na wachezaji wamekuwa wakidaiwa kuchukua pesa na ‘kulegeza kamba’ uwanjani wakati wa mechi zao ili kuzibeba timu nyingine.

Hizo ndiyo tuhuma za miaka na miaka katika soka la Bongo.

Ndiyo maana matokeo ya mechi chache ambazo timu ndogo hupambana kishujaa kutafuta ushindi na hata ‘kuangusha kabati’, huwa ni stori kubwa.

Huwa stori kubwa mtaani kwa sababu matokeo ya ‘sungura kumkaba tembo’ si mambo ya kawaida katika soka la Bongo. Ni mara chache sana kutokea matukio ya hivyo.

Lakini wapenda soka wa kweli, tunapenda kuona timu zikicheza kishujaa kama Shooting walivyocheza dhidi ya Yanga.

Tunapenda kuona wakicheza hivyo pia dhidi ya timu nyingine, isiwe kukamia mechi chache tu, japo kufungwa ni matokeo ya kawaida, ila unafungwaje ni jambo linalozingatiwa sana.

Tunahitaji kuona Ligi Kuu ya Tanzania Bara ina timu zinazopambana kiuhalali uwanjani kusaka matokeo.

Ni kupitia njia hii ndiyo tunaweza kuinua soka letu la Bongo.

Kwa miaka mingi Tanzania imeshindwa kufika japo nafasi ya 100 katika viwango vya ubora wa soka la dunia vinavyotolewa na FIFA, mara zote tumekuwa katika nafasi ya 120 na kuendelea na sasa tuko katika nafasi ya 137.

Msimu uliopita, Ligi Kuu ya Bara ilikosa mdhamini mkuu na kuchangia kuidhoofisha kutokana na timu nyingi kushindwa kusafiri kwa wakati kuelekea katika vituo vya mechi zao, wachezaji kukosa mishahara na hata kukosa pesa ya malazi.

Vodacom wamepatikana kudhamini Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, japo udhamini hauwezi kumaliza matatizo ya klabu zote, lakini tunatarajia matokeo mengi ya kushangaza kama ya Shooting na Yanga juzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz