Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

YALIYOJIRI MACHI 2018: Yanga yavunja mwiko Nangwanda Mtwara

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwaka 2018 unaelekea ukingoni na matukio mbalimbali ya michezo ya kufurahisha na kuhuzunisha yalitokea ndani ya mwaka huu.

Gazeti hili linakuletea matukio mbalimbali yaliyojiri ndani ya mwezi Machi.

Machi Mosi

Yanga yavunja mwiko Mtwara

Baada ya kukaa muda mrefu bila kupata ushindi dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, hatimaye Yanga ilipata ushindi ikivunja mwiko kwenye uwanja huo kwa ushindi wa 2-1.

Tangu Ndanda ipande daraja kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2014 haikuwahi kushindwa na Yanga kwenye uwanja huo hadi Machi Mosi huu waliposhinda.

Machi Mosi

Lundenga aitema Miss Tanzania

Waandaaji wa muda mrefu wa shindano la Miss Tanzania, Lino International Agency chini ya uratibu wa Hashim Lundenga walibwaga manyanga kuendesha shindano hilo na sasa linaendeshwa na mrembo wa zamani ‘Miss Tanzania 1998’ Basila Mwanukuzi.

Machi 5

Waamuzi Watanzania wawekwa kitanzini CAF

Waamuzi wanne kutoka Tanzania walijikuta matatani baada ya kutakiwa aandike utetezi kwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kutuhumiwa kupanga matokeo katika mchezo wa Rayon Sports ya Rwanda na Lydia Ludic ya Burundi ambao Rayon ilishinda bao 1-0.

Viongozi wa Lydia Ludic ndio walioibua tuhuma hizo kwa waamuzi hao wakisema walipanga matokeo baada ya viongozi wa Rayon kuonekana wakiingia usiku katika chumba cha mmoja wa waamuzi hao.

Waamuzi walioingia matatani ni Israel Nkongo, Frank Komba, Mfaume Ally na Sudi Lila.

Machi 7

Mvua, umeme vyaitibulia Simba

Mvua kubwa iliyoanza kunyesha dakika ya 78 ilisababisha mchezo wa hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na Al Masry kusimama kwa dakika zaidi ya 10 kabla ya mwamuzi wa mchezo huo Thando Helpus kutoka Afrika Kusini ilibidi asimamishe mchezo kutokana na mvua kuwa kubwa zaidi na umeme kukatika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Machi 8

Kigogo TSA ang’olewa

Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhan Namkoveka aliondolewa katika nafasi hiyo na Baraza la Michezo Tanzania (BMT), baada ya mkutano mkuu wa Chama hicho kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.

Machi 9

Ulimwengu azua balaa kuitwa Stars

Baada ya kocha Salum Mayanga kumjumuisha Thomas Ulimwengu katika kikosi cha Taifa Stars, kwa ajili ya michezo ya kirafiki, mashabiki na wadau wa soka walihoji amemuita vipi wakati hana timu kwa muda mrefu.

Hii ilitokona na Ulimwengu kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi na hakuwa na timu kwa miezi sita.

Hata hivyo, Mayanga alijitetea kwa kusema mchezaji huyo amepona na kiwango chake kipo vizuri akiwataka wadau kumpa muda ili athibitishe ubora wake.

Machi 9

Serikali yawabana wanariadha

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liliweka utaratibu mpya kwa wanariadha wanaokwenda kushindana nje ya nchi, kwa kutakiwa kupewa kibali Baraza hilo na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ikitoa barua siku 14 kabla ya safari.

Machi 14

Nidhamu yamng’oa mwanariadha

Mwanariadha Augostino Sulle aliondoleawa kwenye timu ya Taifa iliyokuwa ikijiandaa na mashindano ya Jumuiya ya Madola kwa utovu wa nidhamu. Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na Baraza la Michezo Taifa (BMT) walikubaliana kumuondoa Sulle, kwa kugoma kufanya mazoezi na wenzake huko Sakina nje kidogo ya jiji la Arusha.

Machi 15

Wambura afungiwa maisha

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Michael Mwambura alifungiwa maisha na Kamati ya Maadili ya Shirikisho hilo iliyo chini ya mwenyekiti Hamidu Mbwezeleni.

Wambura alifungiwa kwa makosa matatu ikiwemo kupokea na kuchukua fedha za TFF za malipo ambayo hayakuwa halali, kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya Jecks System Limited na kufanya vitendo vinavyoshushia hadhi shirikisho hilo.

Machi 17

Yanga, Simba zaaga mashindano kimataifa, Yanga ilitolewa Ligi ya Mabingwa Afrika na Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1, wakati Simba ilitolewa Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 2-2 dhidi ya Al Masry ya Misri, zilitoka 2-2 nyumbani na kutoa suluhu ugenini.

Machi 21

Yanga yasalimu amri kwa Azam TV

Baada ya mvutano wa muda mrefu hatimaye Yanga iliamua yaishe na kukubali kuingia mkataba wa udhamini na kituo cha television cha Azam cha jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo Charles Mkwasa alisema mkataba huo utakuwa wa miaka mitatu, akisema wamebaini kuwa hawataweza kuendelea kuukataa mkataba huo wakati soka la sasa nchini limeingia katika mfumo wa kidigitali.

Alisema hiyo ni fursa nzuri kwao kujiingizia kipato na pia kuitangaza klabu kwani watakuwa na Yanga TV kwenye televison hiyo, ambayo wataitumia kuwasiliana na wanachama na mashabiki wao nchi nzima kwa haraka.



Chanzo: mwananchi.co.tz