Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

YALIYOJIRI AGOSTI 2018: TFF yamleta kocha Amunike kuinoa Taifa Stars

33654 MATUKIO+PIC Tanzania Web Photo

Thu, 27 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Agosti 6- Amunike atangazwa kocha mpya Taifa Stars

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimtangaza mchezaji wa zamani wa Barcelona na Nigeria ‘Super Eagles’ Emmanuel Amunike , kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars.

Hadi anateuliwa kumrithi Salum Mayanga, Amunike alikuwa na shahada ya Uzamili ya ukocha kutoka Shirikisho la Soka la Barani Ulaya (Uefa) pia ana leseni Daraja A ya ukocha kutoka Uefa.

Mbali ya Barcelona, Amunike amewahi kuzitumikia pia timu za Sporting Lisbon ya Ureno pamoja na miamba ya sokia nchini Misri timu ya Zamalek.

Agosti 10

Chilunda aenda kukipiga Hispania

Mshambuliaji chipukizi wa Azam FC, Shaban Iddi Chilunda alijiunga na klabu ya CD Tenerife inayocheza Ligi Daraja la Kwanza nchini Hispania.

Mchezaji huyo alisaini mkataba wa mkopo wa miaka miwili na kujiunga na mchezaji mwenzake wa zamani wa Azam Farid Mussa aliyekuwa wa kwanza kusajiliwa na klabu hiyo.

Agosti 11

Cannavaro aagwa Yanga

Nahodha wa zamani wa Yanga, Zanzibar Heroes na Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alistaafu rasmi kucheza soka na kuagwa na timu yake katika mchezo maalumu uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Cannavaro alistaafu baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka 12 na aliamua kukabidhi jezi yake yenye namba 23 mgongoni kwa beki chipukizi wa timu hiyo Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye pia ni Mzanzibar mwenzake.

Agosti 13

Mwanariadha apandishwa cheo Polisi

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro alimpandisha cheo mwanariadha Fabian Nelson kutoka Konstebo na kuwa Koplo baada ya kutwaa medali ya dhahabu akivunja rekodi ya mbio za mita 5000 katika michezo ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi Ukanda wa Afrika Mashariki (Eapcco).

Fabian alitumia dakika 13: 45: 99 akiwashinda wanariadha wa Jeshi la Polisi la Kenya na Uganda ambapo Tanzania ilishika nafasi ya pili katika ushindi wa jumla.

IGP Sirro alisema mwanariadha huyo amekuwa akionyesha juhudi katika mbio ndefu jambo ambalo limekuwa likileta sifa kwa Jeshi la Polisi na nchi kwa ujumla.

Agosti 14

TFF yaongeza wachezaji wa kigeni Ligi Kuu

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka saba hadi 10, Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia alisema wachezaji wote 10 wanaruhusiwa kuanza katika mchezo mmoja kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi la timu husika.

Agosti 16

Ligi Kuu Bara yakosa mdhamini

Bodi ya Ligi ilitangaza Ligi Kuu Bara msimu huu itaanza kuchezwa bila mdhamini mkuu baada ya kampuni ya Vodacom iliyokuwa ikidhamini Ligi hiyo kwa miaka mitatu kwa mkataba wa Sh 6.6 bilioni kujitoa.

Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, alisema ligi ya msimu huu itaanza bila ya kuwa na mdhamini mkuu kwani hawajafikia makubaliano na kampuni yoyote.

Jambo hilo lilionekana kuzichanganya timu nyingi kwani mara nyingi zilitegemea kupokea fedha za awali kutoka kwa wadhamini kufanikisha mahitaji mbalimbali ikiwemo usafiri.

Agosti 18

Yanga yatolewa Shirikisho

Timu ya Yanga ilitolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufanya vibaya katika hatua ya makundi, ikifungwa na Gor Mahia ya Kenya mabao 4-1 ugenini kabla ya kuchapwa 3-2 nyumbani, pia ilifungwa na USM Alger ya Algeria mabao 4-0 ugenini na kutoka sare ya bao 1-1 na Rayon Sport ya Rwanda.

Hata hivyo kilichoigharimu Yanga ni ukata kwani katika mechi hizo baadhi ya wachezaji akiwemo nahodha, Kelvin Yondan, kipa Beno Kakolanya na wachezaji wengine waligoma kucheza.

Agosti 18

Simba yatwaa Ngao ya Jamii

Simba ilianza vizuri ufunguzi wa msimu huu wa Ligi ilipotwaa Ngao ya Jamii kwa kuilaza Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 2-1, ikiwa ni miezi mitatu tangu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Agosti 28

Kigogo TFF afungiwa maisha

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na msimamizi wa ligi kituo cha Shinyanga, Mbasha Matutu alifungiwa kujihusisha na soka maisha.

Kamati ya Madili ya TFF iliyo chini ya wakili Hamidu Mbwezeleni ilimfungia Matutu kwa madai ya ubadhirifu, kughushi na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika mechi kati ya Stand United na Simba na Stand United dhidi ya Prisons.

Agosti 30

Wachezaji wa Simba watimuliwa Stars

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike aliwatimua kambini wachezaji sita wa Simba kwa kuchelewa kuripoti kambini wakati timu hiyo ikijiandaa kwa mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Uganda.

Wachezaji hao ni Shiza Kichuya, Erasto Nyoni, John Bocco, Jonas Mkude, Shomari Kapombe na Hassan Dilunga, ingawa baadaye ilibainika kuwa walichelewa kupata taarifa za wito wa kujiunga na wenzao kambini.



Chanzo: mwananchi.co.tz