Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili wapya watua Simba

Wapya Pic Data Wawili wapya watua Simba

Sat, 4 Sep 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

WACHEZAJI wapya wawili wa Simba, Kibu Denis aliyetokea Mbeya City na Jeremia Kisubi wa Tanzania Prison, wameripoti kambini juzi Jumatano jioni na tayari wameanza kukiwasha.

Kibu na Kisubi bado hawajatambulishwa kuwa ni wachezaji wapya wa Simba kama ilivyokuwa kwa wengine kumi, kutokana na sababu mbalimbali za msingi ambazo ziliwakwamisha hata kwenda kambini Morocco ikiwemo madai kwamba uraia wao unachunguzwa.

Kisubi ndio alikuwa wa kwanza kufika katika kambi ya Simba Jumanne, akivalia nguo zake za nyumbani hakufanya mazoezi na wachezaji wengine ila alikwenda kuongea na Meneja, kisha baada ya mazungumzo hayo kumalizika aliondoka.

Mapema mchana wa Jumatano Kisubi na Kibu waliwasili kambini hapo na jioni walifanya mazoezi ya gym na wachezaji wengine kisha mara baada ya kumaliza walipewa ruhusa ya kurudi majumbani kwao kupumzika na kusubiri ratiba nyingine ya siku zinazofuata.

Baada ya kurejea nchini kikosi cha Simba wakitokea Rabat, Morocco kwenye mazoezi, tayari wameanza maandalizi mengine kwa ajili ya michezo ya kimashindano ukiwemo ule wa Septemba 25, Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

Simba wanafanya mazoezi ya nguvu gym, kwa siku yanafanyika kwa awamu moja jioni. Katika mazoezi hayo kocha wa viungo, Adel Zrane ndio anasimamia shoo nzima ingawa kocha mkuu, Didier Gomes nae anakuwepo katika awamu hiyo ya mazoezi magumu ambayo wanaendelea nayo.

Wachezaji wa Simba ambao hawapo katika majukumu ya timu za taifa kuanzia Jumatatu wataingia kambini mchana kisha kufanya mazoezi ya gym Jioni, iliyopo ndani ya kambi yao Mbweni na baada ya hapo kila mmoja anapewa ruhusa ya kwenda kwake.

Sambamba na hilo Mwanaspoti linafahamu kocha wa Simba, Gomes kabla ya kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki katika kilele cha Simba Day, anataka michezo mingine miwili au mitatu ya kirafiki ili kuwapima vijana wake. Miongoni mwa wachezaji waliopo katika ratiba hiyo ya mazoezi ni Bocco, Dilunga, Gadiel Michael, Ally Salim na Hennock Inonga.

Wengine Kibu, Kisubi, Sadio Kanoute, Pape Ousmane Sakho, Bernard Morrison, Yusuph Mhilu, Abdulsamad Kassim, Ibrahim Ajibu, Jimsony Mwanuke na Dancun Nyoni.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz