Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania wazidi kutikisa kimataifa

12803 Pic+samatta TanzaniaWeb

Mon, 20 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Washambuliaji wa Tanzania, Saimon Msuva anayeichezea Difaa El Jadida ya Morocco na Mbwana Samatta anayekipiga Ubelgiji kwenye klabu ya KRC Genk wameendelea kuwa wachezaji muhimu kwenye vikosi vyao wikiendi iliyoisha.

Msuva ndiye aliyefufua matumaini ya Difaa El Jadida kutinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupachika bao Jumamosi kwenye mchezo ambao waliifunga MC Alger ya Algeria kwa mabao 2-0.

Matokeo hayo, yameifanya klabu hiyo anayoichezea Msuva kufikisha pointi tano na kusogea hadi kwenye nafasi ya pili huku wakisaliwa na mchezo mmoja na vinara wa Kundi E, TP Mazembe ambao utawalazimu kushinda ili kutinga 16 bora. TP Mazembe ambao tayari wametinga katika hatua wakijikusanyia pointi 11.

Msuva alisema: “Wao wameshafuzu kwa hiyo wanaweza kuweka kikosi dhaifu japo hizo siyo hesabu zetu maana kwa namna yoyote ile tutaenda kutafuta matokeo.”

Nahodha wa Taifa Stars, Samatta naye aliibeba KRC Genk katika michezo miwili ya raundi ya tatu ya kuwania nafasi ya kuingia katika makundi ya Europa Ligi dhidi ya Lech Poznan ya Poland.

Katika michezo hiyo miwili ya nyumbani na ugenini, Samatta alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa jumla ya mabao 4-1.

Mechi ya kwanza baina ya Genk na Lech Poznan ulimalizika kwa timu hiyo anayoichezea Samatta wakishinda kwa mabao 2-0, mchezo wa marudiano ugenini wakashinda 2-1 huku Samatta akifunga bao moja kwenye kila mchezo.

Naye mtoto wa mchezaji wa zamani wa Kikwajuni ya Zanzibar, Roberto Nditi ameweka rekodi ya kufunga bao lake la kwanza kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu England kwa vijana wa U-18.

Roberto ambaye ni beki wa kati anayeichezea Reading alifunga bao hilo dakika ya 39 dhidi ya Norwich City ya U-18.

Naye kocha wa CD Tenerife ya Hispania, Joseba Etxeberria ameelezea kukunwa na soka ya Mtanzania, Shabaan Idd Chilunda baada ya kufunga mabao matatu kwenye mazoezi ya timu hiyo ambayo leo inaanza msimu dhidi ya Club Gimnàstic de Tarragona.

Chanzo: mwananchi.co.tz