Wakati mashindano ya mbio za Tigo Kili Half Marathon yakitarajiwa kufanyika Februari 26 mkoani Kilimanjaro, washiriki wametakiwa kujiandaa.
Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Tigo, Woinde Shisael amesema hayo leo Jumanne Februari 14, 2023, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Usajili umeshafungwa baada ya nafasi kujaa kwa mbio za Km 42 na 21.”
Shisael amesema kilichobaki sasa ni washiriki kuchukua namba zao kuanzia mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam na kuendelea kufanya mazoezi tayari kwa mashindano wiki ijayo.
“Kazi ya utoaji namba itaanzia Dar es Salaam Februari 18 na 19 mwaka huu katika Viwanja vya Mlimani City kuanzia saa sita mchana hadi saa 12 jioni. Baada ya Dar es Salaam, kazi hiyo itahamia Arusha katika Hoteli ya Kibo Palace Februari 21 na 22 kuanzia saa nane mchana hadi saa moja jioni,” amesema Shisael.
Pia, amesema kituo cha mwisho ni Moshi Mjini kazi ya utoaji namba itafanyika Februari 23 kuanzia saa sita mchana hadi saa 11 jioni, Februari 24 itaanza saa nne asubuhi hadi saa 12 jioni na Februari 25 kazi itakuwa saa tatu asubuhi hadi saa 11 jioni katika Uwanja wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU).
Ametoa wito kwa washiriki wote kujitokeza kuchukua namba zao kwa wakati ili kuepusha usumbufu.