Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapindua meza Simba, Yanga

Wapindua Pic Data Wapindua meza Simba, Yanga

Fri, 21 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

BAADHI ya wachezaji wazawa wameamua kuondoa dhana potofu ndani ya kikosi cha Simba na Yanga, kwa kuonyesha ushindani mkali wa namba mbele ya wageni.

Simba na Yanga kuna nafasi ambazo zimemilikiwa na wazawa na wamekuwa wakileta presha pindi wanapokosekana kwa baadhi ya mechi ngumu.

Kikosi cha Simba, bandika bandua beki ya kushoto utamkuta nahodha msaidizi Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kulia Shomari Kapombe, kipa Aishi Manula ni kwa dharura atacheza Beno Kakolanya anayeonekana hana nafasi ya kuaminiwa moja kwa moja kikosi cha kwanza, tangu ajiunge na Simba akitokea Yanga.

Kapombe na Shabalala kabla ya Simba kuweka wazi kuwasainisha mikataba mipya, iliwapa presha mashabiki wao baada ya kupata taarifa za chinichini kwamba watajiunga Yanga, hilo linathibitisha umuhimu wao na namna ilivyo wanavyopambana kikosi humo.

Ikitokea wachezaji hao wanapata tatizo litakalowafanya wakose mechi muhimu, kocha Didier Gomes atalazimika kuwatumia Gadiel Micheal kucheza nafasi ya Tshabalala na David Kameta ‘Duchu’ badala ya Kapombe ambao wanaonekana kutoaminiwa.

Wakati Yanga wachezaji wazawa waliopata heshima ya kuaminiwa kikosi cha kwanza na wamekuwa wakicheza kwa kutegemewa mechi nyingi ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ Metacha Mnata na Shomari Kibwana ambaye tangu ajiunge nao akitokea Mtibwa Sugar, anacheza kikosi cha kwanza.

Ndani ya kikosi hicho, Fei Toto ndiye anategemewa zaidi nafasi yake na kuna wakati mwingine anabadilishiwa majukumu, akiwemo Tonombe Mukoko kwenye kikosi anacheza kiungo wa juu, akikosekana Mkongomani huyo anacheza kiungo ya chini.

NENO LA WADAU

Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Kasongo Athumani alisema wachezaji hao wamejitambua na kuheshimu kazi wanayoifanya, jambo linalowapa thamani na kuonekana wana umuhimu ndani ya timu hizo.

“Kama kuna kitu natamani kukiona ni wachezaji wazawa wengi waonyeshe thamani yao mbele ya wageni, inawezekana na ndio maana hao wengine wanapata nafasi ya kucheza na unaona presha inavyokuwa kubwa pindi wanapokuwa wanakosekana,” alisema.

Kwa upande wa straika wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema kuwa; “Kama hao wengine wameweza, wengine wanashindwa wapi, kusajili wachezaji wa kigeni kuna maana kwamba waongeze ushindani na sio wao walale na kuona hawana kazi ya kufanya hilo sio sawa, kwanza wakijituma timu yetu ya Taifa Stars itakuwa imara.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz