Klabu ya Dar Jogging kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimimba Swimming Promotions ya Kigamboni imeandaaa mafunzo ya kuogelea kwa lengo la kuhamasisha watu kushiriki kwenye mchezo huo, yanayotarajiwa kushirikisha waogeleaji 100.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhan Namkoveka amesema mafunzo hayo yatahamasisha kuogelea kwa kutumia bahari, kujifunza usalama wa maji, kuzuia na kupunguza vifo vinavyotokana na maji lakini pia kuogelea kwa afya ya mazoezi ya kwenye maji.
"Faida hizi pamoja na zingine zitapatikana kama mtu atakuwa na uwezo wa kujua kuogelea na kumsaidia kujiokoa mwenyewe endapo atapata tatizo lolote akiwa baharini," amesema.
Amesema mafunzo hayo ya siku tano yatafunguliwa Julai 26 kwenye fukwe za chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere na fukwe za Navy zilizopo Kigamboni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
"Mafunzo haya pia yatatumika kupata waogeleaji kwa ajili ya mashindano ya baharini au kwenye maziwa (open water swimming) ambayo majina yao yatawasilishwa kwenye Kamati ya ufundi ya Chama cha kuogelea Tanzania (TSA) kwa taratibu zingine ikifaa.
"Dar Jogging tayari tumefanya vikao mara mbili na Chama cha Kuogelea Tanzania kwa ajli ya mafunzo haya, lakini pia tutayatumia kama sehemu ya kusheherekea miaka 20 ya klabu yetu tutakayoadhimisha Agosti 8 kwa kushiriki mbio za barabarani," amesema.
"Bajeti yetu ili kufanikisha mafunzo haya ni Sh 12.5 Milioni, ambazo tunawaomba wadau wetu mbalimbali watusapoti kwenye hili," amesema Namkoveka na kuongeza.
"Tunatarajia kuwa na waogeleaji wasiopungua 100 kushiriki mafunzo haya kwa jinsia zote, lakini watakaoruhusiwa kushiriki ni wa kuanzia miaka 10 kuendelea.