Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 600, kati ya hizo 300 zipo kwenye mfumo wa kisasa wa umwagiliaji.
Akizungumza katika ziara yake ya kukagua mchakato wa kulifufua shamba hilo lililoanzishwa mwaka 2008/9, Bashe alisema shamba hilo liliacha kuzalisha mwaka 2015 na alipolitembelea awali aliagiza wamiliki kusafisha maeneo yao ili kufufua kilimo hicho.
“Nilishatoa muda kila mtu asafishe shamba lake, lakini kuna watu 86 hawakuonekana na hawajasafisha, pia kulikuwa kuna watu wakubwa wanamiliki mashamba, naomba muwaondoe na mashamba hayo yagawiwe kwa wakulima wengine ambao wapo 'serious' kwa ajili ya kushirikiana katika safari ya kulifufua shamba hili," alisema.
"Ninawaambia atakayenizuia kuwaondoa watu hao labda awe ni Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango na Waziri wangu wa kilimo, Prof. Adolf Mkenda, hao wanne tu ndio wanaoweza kunizuia kuwaondoa na hakuna mwingine maana maamuzi tulishafanya na tulishatoa muda, kama walifikiri tunafanya sanaa hapa.”
Aidha, alisema awamu ya kwanza ya ufufuaji wa shamba hilo umekamilika na wanakwenda kuanza awamu ya pili.
Alisema katika shamba hilo kulikuwa kuna visima vitatu vya maji ambavyo vilikuwa vinatoa maji lita 40,000 hadi 50,000 kwa saa na bwawa linahifadhi lita 41,000 na wameanza kuvifufua.
Bashe alitoa siku 15 kuhakikisha kazi zote zinakamilika ili mradi huo uanze mwaka huu.
"Tulijiwekea lengo na wakulima hapa kwamba lazima mwaka huu shamba hili liamke na hatua za awali inatia moyo wakulima wameungana wanashinda wenyewe hapa shambani kwa kushirikiana na wataalam wa Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kulifufua na kama mnavyoona tayari bwawa limesha karabatiwa na maji yanaingia,” alisema.
Hata hivyo, Bashe alisema uwekezaji huo unaofanywa na serikali wakulima watarejesha fedha zote baada ya uzalishaji kuanza.
Alisema baada ya shamba hilo kufufuliwa watakaa na watu wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ili watengeneze miundombinu itakayowawezesha wakulima kuuza mchuzi badala ya kuuza matunda yazabibu ili kilimo chao kiwe na tija.
Awali, akitoa taarifa ya ukarabati wa bwawa na visima katika shamba hilo, Mhandisi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Dodoma, Raphael Laizer, aliiomba serikali iwasaidie fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kumalizia ukarabati.