Kwa sasa Instagram imekuwa zaidi ya jukwaa lingine la mitandao ya kijamii. Facebook (sasa Meta) imevunja vizuizi vyote vya kimataifa na vya umri kwa kumuunganisha kila mtu. Uchunguzi unaonyesha kuwa kwa wastani, mtumiaji wa Instagram hutumia kama dakika 28 juu yake.
Vile vile imefungua njia kwa bidhaa na makampuni makubwa hadi madogo kuwezesha watu kuzifikia. Instagram pia ni mahali ambapo watu mashuhuri hutumia zaidi na mashabiki wao na kupata maoni ya maisha ya kila siku ya nyota wao.
Kuanzia nyota wa filamu hadi kwa wanamichezo, karibu kila mtu hutumia Instagram kwani inachukuliwa kuwa njia bora zaidi. Licha ya kuungana na mashabiki na kuchapisha kuhusu maisha yao ya kila siku, watu mashuhuri pia hupata malipo mazuri kwa machapisho yao.
Makala haya inawachambua wanamichezo watano wanaolipwa fedha nyingi zaidi kwa chapisho moja kwenye Instagram, hawa hapa...
#5. LeBron James (Mpira wa Kikapu) – Dola 474,000
LeBron James maarufu kama Mfalme James ndiye mchezaji maarufu zaidi wa mpira wa kikapu nchini Marekani, NBA.
Anajivunia zaidi ya wafuasi milioni 102 kwenye Instagram. Mpira wa Kikapu ni mchezo mzuri na hauna umaarufu mkubwa sana nje ya Marekani. Hata hivyo, haikuwa kikwazo kwa LeBron James kujulikana ulimwenguni kote.
Mzaliwa huyo wa Ohio, anaingiza takriban dola 474,000 kwa kila chapisho la Instagram. LeBron James anapata wafuasi wengi kwa mfumo wake wa mazoezi ya mwili.
#4. Virat Kohli (Kriketi) – Dola 680,000
Nahodha wa Timu ya Kriketi ya India, Virat Kohli anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi wa wakati wote wa mchezo huo. Takwimu zake za kuvutia zinaambatana na sifa yake na hiyo inamfanya kuwa mmoja wa nyota wa michezo wanaofuatiliwa zaidi kwenye Instagram.
Kriketi, ukiwa ni mchezo mwingine mzuri, hauwezi kufurahiwa kama ilivyo kwa ule wa soka. Licha ya hayo, Virat Kohli anajivunia wafuasi wengi zaidi kuliko wanasoka wengi. Kohli ana wafuasi milioni 168 na ndiye mtu anayefuatiliwa zaidi nchini India.
#3. Neymar Jr (Soka) – Dola 824,000
Tangu akiwa kule Santos, Neymar Junior, mara zote amekuwa gumzo. Alianza kama mchezaji kijana mwenye maajabu na ujuzi wake wa kucheza katika ligi ya Brazil. Aliendelea kutawala Ulaya pamoja na Lionel Messi na Luis Suarez akiwa na Barcelona. Maisha ya Neymar yamezidi kukua na kuwa juu.
Umarufu zaidi ulikuja baada ya Mbrazil huyo kuhamia PSG kama mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka. Alitua pale Paris mwaka 2017 kwa kitita cha euro milioni 222. Mashujaa wake wa ndani na nje ya uwanja wamemfanya Neymar kuwa mmoja wa nyota wa michezo wanaotazamwa zaidi kwenye sayari hii.
Pamoja na kuwa mwanasoka stadi, Neymar pia anachukuliwa kuwa mfano wa mitindo ya kisasa. Mitindo yake ya kunyoa nywele kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, imemfanya kuongeza umaarufu wake. Staili yake ya kuvaa pia huigwa na vijana wengi kote duniani. Neymar ana wafuasi milioni 165 kwenye Instagram na analipwa dola 824,000 kwa chapisho moja.
#2. Lionel Messi (Soka) – Dola 1,169,000
Lionel Messi na rekodi zinakwenda sambamba, si ndiyo? Katika ulimwengu huu wa kuvutia wa kandanda, raia huyo wa Argentina amejidhihirisha katika masuala ya ujuzi na fedha. Messi amebaki kuwa mmoja wa wanamichezo wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani.
Sehemu kubwa ya mapato yake hutokana na mishahara, mikataba binafsi na bila shaka, Instagram. Inaripotiwa kuwa nahodha huyo wa zamani wa Barcelona anaingiza takriban dola 1,169,000 kwa kila chapisho la Instagram na ana wafuasi milioni 281.
Ujuzi wa hali ya juu wa Messi na ushindani wake na Cristiano Ronaldo umemfanya kuwa mwanasoka maarufu zaidi wakati wote.
#1. Cristiano Ronaldo (Soka) – Dola 1,604,000
Akiwa na wafuasi milioni 367, Cristiano Ronaldo ndiye mtu anayefuatiliwa zaidi kwenye Instagram. Hahitaji utangulizi wowote ili kuhalalisha umaarufu wake mtandaoni. Ronaldo ndiye kielelezo cha utimamu wa mwili na akiwa na umri wa miaka 36, anacheza kama kijana wa miaka 22.
Vile vile humfanya kuwa mtu wa kuigwa kwa utimamu wa mwili na hivyo nahodha huyo wa Ureno amekuwa akifutiliwa sana na wapenda mazoezi. Chapa nyingi za kimataifa zimempata mwanasoka huyo wa zamani wa Real Madrid kama balozi wao, huku Nike ikiwa kinara.
Ronaldo anaishi maisha ya unyenyekevu nje ya uwanja na hutumia muda wake mwingi kuzunguka na familia yake. Chapisho la Ronaldo, ambalo alitangaza ujauzito wa mpenzi wake, ni chapisho la pili kupendwa zaidi kwenye Instagram.