Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanamichezo wamlilia Mkapa

0d7da8b73cba4461a831f36554a8aace Wanamichezo wamlilia Mkapa

Sat, 25 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WADAU wa michezo nchini wamemlilia Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyefariki dunia jana usiku katika hospitali jijini Dar es Salaam, wakisema wamepoteza kiongozi mahiri.

Rais John Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia jana. Miongoni mwa mambo makubwa ambayo wadau wa michezo wanamkumbuka Rais Mkapa katika uongozi wake ni ujenzi wa Uwanja wa Taifa uliozinduliwa Septemba 2007 na mchezo kwanza wa kimashindano kuchezwa ulikuwa wa kufuzu michuano ya Mataifa Afrika (AFCON) kati ya Tanzania na Msumbiji ambao Tanzania ilifungwa 0-1.

Bondia mstaafu wa ngumi za kulipwa, Mbwana Matumla ‘Snake Boy’ amepokea kwa masikitiko kifo cha Mkapa na kusema hatomsahau kwa jinsi alivyokuwa anapenda kuenzi wanamichezo na michezo.

Matumla alisema jana kuwa, mwaka 1995 alimpiga bondia Mwenda Chama kutoka Zambia na mwaka 1999 alimpiga bondia Paulo Pizzamiglio raia wa Italia katika ubingwa wa dunia na mara zote alialikwa Ikulu na Rais Mkapa kumpongeza.

Alisema mwaka 1999 Rais Mkapa alimpa tuzo ya mwanamichezo aliyetukuka kwa kuliletea sifa taifa, na kwamba alimwambia michezo ni mizuri kwa sababu inatangaza nchi pale wanapofanya vizuri.

Naye Kaimu Mhariri wa gazeti hili Mgaya Kingoba, alisema kwa mara ya kwanza aliingia Ikulu baada ya Rais Mkapa kumwalika bondia Matumla Ikulu mwaka 1996 na kusema Mkapa alisema anapenda michezo tofauti na watu wanavyomfikiria.

Alisema, Mkapa alisema anafuatilia michezo kwa karibu tatizo lake ni kutoonekana uwanjani tu. Ujenzi wa Uwanja wa Taifa Mwaka 2003 wakati Simba inarejea kutoka Cairo baada ya kuitoa Zamalek na kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika siku hiyo pia Rais Mkapa alikuwa akitoka katika ziara nje ya nchi alipofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (wakati huo ulikuwa ukiitwa DIA), alishangaa kukuta umati mkubwa wa watu akamuuliza Mkuu wa Mkoa wa kipindi hicho, Yusuph Makamba; “Umati huu umekuja kunipokea mimi?” Makamba akajibu: “Hapana wamekuja kuipokea Simba sababu imeshinda huko Misri.”

Rais Mkapa alishangazwa na mapenzi ya wananchi wake kwenye soka na akaweka ahadi ya kujenga uwanja wa kisasa ambao ndio huu unaitwa Benjamin Mkapa, ambao leo hii tunajivunia na ni kumbukumbu.

Januari 2003, serikali ilitangaza zabuni na kampuni zaidi ya 11 zilijitokeza lakini zilikuwa na bajeti kubwa tofauti na makadirio ya serikali na Waziri wa Michezo wa wakati huo, Juma Kapuya alisema bajeti ya serikali ilikuwa Dola za Marekani milioni 60. Mchakato uliendelea hadi Juni 2004, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje kwa wakati huo na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alisaini mkataba wa Dola za Marekani milioni 56 na serikali ya China kwa ajili ya ujenzi na kampuni ya Beijing Construction Engineering Group ikaanza ujenzi.

Juni 2006, ujenzi ulikamilika na Kiongozi Mkuu wa China wakati huo, Premier Wen Jiabao alitembelea uwanja huo kabla haujaanza kutumika. Mechi nyingine kubwa zilizochezwa katika uwanja huo ni kati ya Taifa Stars na Brazil mwaka 2010, mchezo ambao Stars ilifungwa mabao 5-0, mingine ni Everton na Gor Mahia, Simba na Sevilla na maveterani wa Real Madrid na Barcelona.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ambao ni wanufaika zaidi wa Uwanja wa Taifa alituma salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli kutokana na msiba huo mkubwa.

Karia anasema TFF imepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa na katika mpira wa miguu, Mkapa ataendelea kukumbukwa siku zote kwa kuacha kumbukumbu ya Uwanja mkubwa wa Taifa unaofahamika Benjamin Mkapa na unaowafanya watembee mbele katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Kwa niaba ya TFF, natoa pole kwa Rais John Magufuli, Watanzania, familia na wote walioguswa na msiba huo, pumzika kwa amani shujaa wetu Benjamin Mkapa,” alisema Karia.

“Bado ni ngumu kukubali kwamba Mzee Mkapa hatunaye tena, pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwa ujumla kwa msiba huu mzito, Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, tangulia baba, nasi tunakuja” ameandika Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’.

“Kwake tumetoka na kwake tutarejea, watanzania sote tutakukumbuka upumzike kwa amani Mstaafu Rais wetu,” ameandika Msanii Mzee Yusuph.

“Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa kiongozi wetu, mlezi wetu na Rais wetu mstaafu Benjamin Mkapa, salamu za pole ziwafikie ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu popote walipo, tupo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu na Mungu awatie nguvu,” ameandika G Nako Warawara.

“Habari ya kusikitisha sana ambayo nimeamka nayo, tumempoteza Rais wa awamu ya tatu Tanzania, Benjamin William Mkapa, pumzika kwa nguvu asante kwa diplomasia yako, mchango wako na huduma zako kwenye jamii,” ameandika Nikki Mbishi.

“Nilipokea habari za Rais Benjamin Mkapa kwa huzuni kubwa, mtu wa kanuni, dhamira thabiti na uadilifu, rehema yangu kwa familia yake, marafiki, wanachama wa CCM, na Tanzania nzima kwa ujumla, pumzika kwa amani Mzee Mkapa,” ameandika Wakazi. “Pumzika kwa amani Benjamin,” ameandika Mbwana Samatta.

“Nawapa pole Watanzania na familia yake. Alikuwa na maono na alikuwa mkweli na alipenda michezo ndio maana alitujengea uwanja ambao sisi riadha na soka tunanufaika sana,” Suleiman Nyambui. Rais Mkapa alizaliwa mwaka 1938 Masasi katika kijiji cha Lupaso mkoa wa Mtwara.

Chanzo: habarileo.co.tz