Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na Baraza la Michezo Taifa (BMT), imeandaa tuzo ya wanamichezo bora wa mwaka 2023 zitakazofanyika Juni 09, 2023 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo, Profesa Madundo Mtambo, amesema hiyo ni mara ya pili kuandaa tuzo hizo na safari hii kuna tofauti kubwa ukilinganisha na tuzo za mwaka jana.
Amesema tuzo zilizofanyika mwaka jana kila mchezo uliofanya vizuri ulipewa fursa ya kuwa na mchezaji bora, ambapo kwa tuzo za safari hii zitakazotolewa ni tuzo za ujumla na sio kwa kila mchezo.
“Mabadiliko haya yanalenga kuongeza ushindani na ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuleta usawa wa thamani kwa michezo yote,kadhalika mabadiliko haya yataongezea thamani tuzo hizi," amesema.
Naye Mwenyekiti wa BMT, Leodeger Tenga amesema dhamira ya tuzo hizo ni kuwaheshimisha wanamichezo kwa kufanya vizuri katika michezo ya kanda, kimataifa Afrika na michuano ya kidunia.