Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliokosa penalti Colombia watishiwa kupigwa risasi

10756 Colombia+pic TanzaniaWeb

Thu, 5 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bogota, Colombia. Wakati Colombia ikiadhimisha miaka 24 tangu mchezaji wake nyota Andres Escobar kuuawa kwa kupigwa rasasi, hofu ya tukio hilo kujirudia imetanda baada ya wachezaji Mateus Uribe na Carlos Bacca kutishiwa kifo.

Wakati mkwaju wa Uribe aliyepiga penalti ya tatu uligonga mwamba, kipa wa England, Jordan Pickford alipangua kiki ya Bacca na kuipeleka timu hiyo kwenye robo fainali ambako itakutana na Sweden Jumamosi wiki hii.

Mitandao ya kijamii ya Colombia imenukuliwa ikiwataka Uribe na Bacca wametakiwa wasikanye ardhi ya Colombia baada ya kukosa penalti kwenye mechi ya hatua ya 16 bora dhidi ya England juzi usiku.

Wachezaji hao walikosa penalti muhimu zilizoiondoa Colombia katika fainali hizo nchini Russia na kuipeleka England robo fainali kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika 120.

Wakati salamu za kutishiwa kuuawa zilitolewa, timu hiyo ilikuwa ikijiandaa kurejea nyumbani, baada ya kutolewa kwenye fainali hizo.

Taarifa za vitisho hivyo, zimetolewa wakati juzi ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kuuawa kwa kupigwa risasi Escobar aliyekuwa beki tegemeo wa kikosi hicho ambaye alijifunga katika moja ya mechi za Colombia kwenye fainali za mwaka 1994 nchini Marekani.

Katika ujumbe uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mashabiki hao uliwataka Uribe na Bacca kujiua wenyewe ama wasubiri kukutana na vifo vya kikatili wataporejea nyumbani.

Mashabiki wa Colombia wanafahamika kwa utukutu timu yao inapotolewa hasa kwenye mashindano makubwa kama Fainali za Kombe la Dunia.

Vitisho hivyo vimekumbusha tukio la Escobar aliyejifunga katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Marekani ambao Colombia ilikuwa ikihitaji ushindi au sare ifuzu hatua ya 16 bora.

Kifo cha Escobar aliyepigwa risasi sita kifuani na wauaji wanaosadikiwa ni wacheza kamari, walidai kuchukizwa na kitendo cha Colombia kuondolewa na walichukua uamuzi huo Julai 2, 1994 siku tano tangu Escobar alipojifunga bao hilo.

Polisi wa Colombia walimnasa mlinzi wa genge la kuuza na kusambaza dawa za kulevya la ‘Colombian Drug Carter’, Humberto Castro Munoz ambaye aliomba radhi na kukiri kuhusika na kifo hicho.

Munoz pia alikuwa ni dereva wa bilionea, Santiago Gallon ambaye inadaiwa alipoteza fedha nyingi, alizoweka kama dau la ubashiri wa matokeo akiipa nafasi nchi yake kuibuka na ushindi dhidi ya Marekani na kufuzu hatua iliyofuata.

Mwaka mmoja baadaye, Mahakama ya Colombia ilimkuta Munoz na hatia ya kumuua Escobar kwa kukusudia na kumpa adhabu ya kifungo cha miaka 43 jela, ambayo hata hivyo ilipunguzwa na kufikia 26 na baada ya kuitumikia kwa miaka 11, aliachiwa huru kwa kile kilichodaiwa kuonyesha tabia njema gerezani.

Kuachiwa kwa muuaji wa Escobar kulizua sintofahamu na maswali mengi nchini humo ambapo Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, ilituhumiwa kuhongwa na Gallon ili kumuachia Munoz ingawa upande wa utetezi ulikosa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Escobar alijifunga alipokuwa kwenye harakati za kuokoa krosi ya kiungo wa Marekani, John Harkes ambapo mpira huo ulimgonga na kuingia wavuni, bao ambalo liliifanya Colombia kufungwa mabao 2-1.

Colombia imeshindwa kuingia nusu fainali kwa mara ya kwanza na kuvuka mafanikio waliyopata kwenye fainali za Brazil ambako ilitolewa hatua ya robo fainali.

Chanzo: mwananchi.co.tz