Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliobeba matumaini ya Tanzania Olimpiki 2024

Watz Olimpiki Waliobeba matumaini ya Tanzania Olimpiki 2024

Mon, 22 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni miaka 60 sasa tangu Tanzania ilipoanza kushiriki michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza mwaka 1964 ,wakati huo ikijulikana kama timu ya Watanganyika.

Tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza Tanzania imetwaa medali mbili tu ambazo zote ilizipata katika michezo ya mashindano hayo iliyofanyika mwaka 1980 huko Moscow,Urusi.

Medali hizo zote zilikuwa za fedha,ambapo moja ilitwaliwa na mwanariadha Suleiman Nyambui,aliyeshika nafasi ya pili katika mbio za mita 5000 na nyingine ilichukuliwa na Filbert Bayi katika mbio za mita 3000.

Mara baada ya hapo,Tanzania imekuwa ikipeleka wanamichezo wake katika mashindano hayo lakini wameshindwa kurudi na medali.

Mwaka huu mashindano hayo yanafanyika Paris,Ufaransa kuanzia Ijumaa ya Julai 26 hadi Jumapili ya Agosti 11 na Tanzania itawakilishwa na wanamichezo Saba ambao ni Alphonce Simbu,Gabriel Geay,Magdalena Shauri, Jackline Sakilu,Collins Saliboko Sophia Latiff na Mlugu Andrew Thomas.

Mwananchi imekufanyia uchambuzi wa nyota hao ambao wamebeba matumaini ya watanzania takribani milioni 60 kwenda kufanya kweli Olimpiki.

ALPHONCE SIMBU

Nyota huyo ana medali moja ya Shaba ya mashindano ya Dunia ambayo yalifanyika London Uingereza mwaka 2017 akitumia muda wa 02:09:51 na medali fedha ya jumuiya ya Madola mwaka 2022 huko Birmingham Uingereza.

Simbu (32) anaenda kushiriki Olimpiki ya tatu katika maisha yake akiwa na rekodi ya kuingia kumi bora mara mbili mfululizo kwenye mashindano hayo ambapo mwaka,2016 akishika nafasi ya tano huko Rio De Jeneiro Brazil kwa muda wa 2:11:15.

“Sina hofu kwasababu naendelea kujipima kwenye mazoezi na naona niko vizuri kwahiyo uwezo wa kushindana nao ninao pia uwezo wa kushinda ninao”,anasema Simbu.

JACKLINE SAKILU

Ni mchezaji kutoka timu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),akiwa na rekodi ya taifa ya nusu Marathoni kwa muda wa 01:06:04,anaenda Olimpiki kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake.

Sakilu (37),anasema licha ya Olimpiki ya Paris kusemekana itakuwa ngumu kwa sababu itawakutanisha mabingwa mbalimbali lakini na yeye anaamini atapambana na kuwa miongoni mwa washindi.

“Kati ya hao wakali naamini na mimi ni mmoja wapo hivyo kamba ndio itaamua”

“Unajua kwenye mashindano lolote linaweza kutokea na kujiamini kwako ndio itakufanya uweze kushinda niseme tu kama uzima utakuwepo kama sasa kitaeleweka”.anasema Sakilu.

GABRIEL GEAY.

Huyu ndie bingwa wa marathoni Tanzania kwa upande wa Wanaume akiwa na rekodi ya masaa 2:03:00 rekodi ambayo aliiweka katika mbio za Valencia marathon zilizofanyika Hispania,Desemba 4,2022 akimaliza wa pili.

Geay ambaye ameweka na kuvunja rekodi yake ya marathoni,akifanya hivyo katika mbio za Milano Marathoni za Italia mwaka 2021 kwa muda wa 2:04:55 kisha kuivunja mwaka 2022 kwa mbio za Valencia kwa masaa 2:03:00 anapewa nafasi ya kushinda kutokana na rekodi yake hiyo nzuri.

MAGDALENA SHAURI

Huyu nae ni bingwa wa marathoni Tanzania kwa upande wa Wanawake akiwa na rekodi ya 2:18:41,ambayo aliiweka kupitia mbio za Berlin Marathon, 23,2023 nchini Ujerumani.mbio ambazo pia zilimpa nafasi ya kufuzu Olimpiki.

Mage (28),anashika nafasi ya 43 kwa wanariadha bora wa kike Dunia,rekodi yake ya marathoni inawapa wadau matumaini makubwa ya kufanya vizuri Olimpiki licha ya kwamba anaenda kushiriki kwa mara ya kwanza.

COLLINS SALIBOKO

Umri wake ni miaka 22 tu lakini tayari amebeba jukumu la kuhakikisha Tanzania inapata medali Olimpiki kwani ana uzoefu wa kimataifa.

Amewahi kufanya vyema katika mashindano ya mita 50,100,200,400,800 na mengine mengi,kumbukumbu nzuri ikiwa ni mwaka 2023,akitumia sekunde 24.43 katika mbio za mita 50 free styles kwenye mashindano ya Dunia yaliyofanyika Fukuoka Japan.

SOPHIA LATIFF

Ndie mchezaji mwenye umri mdogo kabisa kwa wachezaji wa Tanzania ambao wanakwenda kushiriki Olimpiki,umri wake ni miaka 17 lakini rekodi zake ndio zinawafanya wengi kujenga imani na matumaini kwake.

Lattif ana medali kadhaa za dhahabu katika mashindano ya taifa ,miongoni ikiwa ni ile ya ubingwa wa klabu ya mwaka huu mita 50 free styles akitumia sekunde 27.54.

MLUGU ANDREW THOMAS

Umri ni miaka 28 na uzito wa 73kg kazi yake si ya kitoto,ana kazi kubwa ya kwenda kuhakikisha Tanzania inapata medali kupitia mashindano ya Judo ambapo wadau wameweka matumaini makubwa kwake kutokana na ubora wake kwani.

Ameshiriki mashindano makubwa ya kimataifa kama African Senior Championships Individuals ambazo zilifanyika mwezi Aprili mwaka huu nchini Misri ambapo alishika nafasi ya Saba.

Chanzo: Mwanaspoti