Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakimbiaji maarufu duniani kushiriki ‘World's Highest Marathon’ Kilimanjaro

Mbio Marathon Wakimbiaji maarufu duniani kushiriki ‘World's Highest Marathon’ Kilimanjaro

Wed, 4 May 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakimbiaji maarufu duniani wa mbio za uwanda wa juu kutoka nchi 8 wataweka rikodi ya kidunia kwa mara ya kwanza katika mashindano ya ‘Word's Highest Marathon’ ambayo yatafanyika katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

Wakimbiaji hao 15 kutoka nchi za Uingereza, Marekani, Ufilipino,Italia, Polandi, Swazilandi, India na wenyeji Tanzania watashiriki mashindano hayo ikiwa ni tangu mashindano ya aina hiyo yafanyike miaka 30 iliyopita katika Milima ya Evaresti.

Miongoni mwa wakimbiaji maarufu duniani watakaoshiriki mashindano hayo ni Sandi Menchi Abahan kutoka nchi ya Ufilipino na Edoardo Albrighi kutoka nchini Italia.

Akizungumzia tukio hilo Mhifadhi Mwandamizi katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa), Charles Ng'endo amesema kabla ya kufanyika kwa mbio hizo watapanda mlima kwa siku 5 ambapo Mei 9 ndio wataanza kukimbia kutoka kituo cha Cossovo kwenda kilele cha Uhuru.

Amesema katika mbio hizo kutakuwa na mbio za aina tatu; ya kwanza ni kukimbia kilometa 3, kilometa 42 na kisha kilometa 54 kutoka kituo cha Cosovo hadi kilele cha Uhuru ambao mshindi wa mbio hizo atapewa zawadi mbalimbali ikiwemo medali.

"Ndani ya wakimbiaji hawa 15 ambao watakimbia katika Mlima Kilimanjaro wapo wakimbiaji maarufu duniani ambao wamekimbia katika milima mbalimbali na wameweka rikodi kubwa kabisa duniani," amesema Ng'endo.

Amesema ujio wa mbio hizo unatokana na uzinduzi wa filamu ya "Royal Tour" uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii hatua ambayo amesema matunda ya kazi hiyo imeanza kuonekana kutokana na ujio huo mkubwa.

"Sasa hivi tunaanza kuona matunda makubwa kwa kazi ambayo Rais wetu ameifanya ambapo tumepata watalii mbalimbali ambao wanakuja kukimbia na kufanya shughuli mbalimbali za kiutalii, tukio hili litafungua utalii wa kimichezo ndani ya hifadhi yetu na kulifungua soko la utalii wa marathoni,"

Waanzilishi na wakurugenzi wa mbio hizo kutoka nchini Uingereza, David Pickles na Robert Edmond wamesema lengo la kuandaa mashindano hayo ni kuamsha hali ya utalii kimichezo katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro baada ya mbio hizo kufanyika kwa miaka 30 iliyopita katika Milima ya Evaresti.

Pickles amesema miongoni mwa wakimbiaji maarufu duniani ambapo watashiriki katika mashindano hayo ni Sandi Menchi Abahan kutoka nchi ya Ufilipino na Edoardo Albrighi kutoka nchini Italia.

"Watakaokimbia katika mashindano haya ni wakimbiaji ambao wanauzoefu wa kutosha, watu wamejipanga maana ni mara ya kwanza kufanyika mlima Kilimanjaro kutokana na mlima wenyewe ulivyo mrefu na mahali uliopo na itaweka rikodi kwa mara ya kwanza duniani," amesema

Naye Robert Edmond amesema mbio hizo zitafanyika kila mwaka katika mlima Kilimanjaro ili kuijulisha dunia kuwa Mlima Kilimanjaro upo Tanzania.

"Tunategemea siku za mbeleni idadi ya washiriki itaongezeka na watalii watakuja Tanzania kwa wingi kwani ni watu wachache duniani wanaweza kushiriki mbio hizi lakini wapo watakao penda kuja kuona mlima Kilimanjaro,"

Mmoja wa waongoza utalii kutoka kampuni ya Shar Tours, Stanley Wariel amesema wageni hao watapanda mlima Kilimanjaro kupitia geti la Machame na watakuwa na wapagazi zaidi ya 40 na waongoza watalii 10 kwenye mbio hizo.

Chanzo: Mwananchi