Wanariadha Watanzania wamegawana medali za dhahabu na wale Wakenya katika mbio za Mbeya Tulia Marathoni (MTM) iliyofikia tamati leo kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Watanzania, Emmanuel Giniki na Magdalena Shauri walitwaa medali hizo kwenye mbio za kilomita 21 (nusu marathoni) wakati kwenye marathoni (kilomita 42) Wakenya, Erick Kiptoo na Daisy Kipsligati walitwaa ubingwa.
Giniki ametwaa ubingwa kwa wanaume kwenye mbio za kilomita 21 akikimbia kwa saa 1:03:52 huku Magdalena akitwaa ubingwa kwa wanawake akitumia saa 1:12:32.
Kiptoo alikimbia na kumaliza kilomita 42 kwa saa 2:17:53.
Kwenye Mbeya Tulia Marathoni inayoandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust na kudhamiwa na ORYX gesi, CRDB benki, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mbeya Cement, NIC na wadau wengine mbalimbali.
Spika wa Bunge, Dk Tulia aliwaongoza wanariadha wa mbio ndefu za barabarani asubuhi ya leo, akiwa sanjari na viongozi mbalimbali wakiwamo Wabunge na wanariadha nyota wa zamani wakiongozwa na washindi wa Olimpiki, Filbert Bayi na Suleiman Nyambui.
Kwenye kilomita 21, nafasi ya pili ilichukuliwa na Joseph Panga aliyekimbia kwa saa 1:04:15 na Kipruto wa Kenya alhitimisha tatu bora akitumia saa 1:06:15 huku bingwa wa zamani wa dunia, Fabiano Joseph akimaliza wa nane.
Kwa wanawake, Magdalena Shauri aliyekimbia kwa saa 1:12:32 na Marcelina Mbua alimaliza wa tatu akitumia saa 1:14:13 na Jackline Sakilu alihitimisha tatu bora kwa saa 1:15:22 na Failuna Abdi aliingia wa nne akikimbia kwa saa 1:15:52.
Kwenye marathoni, nafasi ya pili ilichukuliwa na Abraham Too aliyekimbia kwa saa 2:18:12 na Rosina Kiboino wote kutoka Kenya alishinda kwa wanawake.
Watanzania, Sarah Ramadhan na Emmanuel Gadiye aliyekimbia kwa saa 2:18:23 walihitimisha tatu bora kwa wanaume na wanawake.
Akifunga mbio ya msimu huu, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema zimekuwa chachu ya wanariadha kujitokeza kwa wingi kushiriki.
"Mbeya Tulia Marathoni imekuwa ikipiga hatua kila mwaka, msimu huu hamasa imekuwa kubwa na tunaamini inakwenda kuleta mabadilliko makubwa kwenye riadha yetu hasa kwa wanariadha wa mbio za uwanjani na wale wa marathoni," amesema.
Huku akiwashukuru kwa upekee baadhi ya wadau walijitokeza kuisapoti mbio ya msimu huu ikiwamo ORYX gesi, benki ya CRDB, TPA, Mbeya Cement na wadau wengine ikiwamo magazeti ya kampuni ya Mwananchi Communications Limited kwa kuihabarisha jamii kwa kina kuhusu mbio hiyo, Dk Tulia amesema, kila mdau aliyeshiriki kwenye mbio hiyo amefanikisha ukarabati wa miundo mbinu ya elimu na afya kwa jamii.
"Lengo la mbio hii ni kuboresha miundo mbinu ya afya na elimu katika mkoa wa Mbeya na maeneo mengine nchini, Taasisi ya Tulia Trust inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika masuala mbalimbali ikiwamo kwenye elimu na afya.
"Tumefanya maboresha katika baadhi ya shule na vituo vya afya hapa Mbeya, lakini pia tulienda Mwanga, tukajenga chumba cha ultra sound kwenye kituo cha afya, hayo ni baadhi tu ya maboresho tuliyofanya kwenye misimu minne ya mbio hii na msimu huu kazi inaendelea, na kila aliyeshiriki kwenye mbio hii ni miongoni wa wanaosapoti lengo hilo la Tulia Trust kwenye Mbeya Tulia Marathoni," amesema.
Washindi wa mbio za mita 100, 200, 400, 800 na 1500 walizawadiwa Sh 500,000 kwa bingwa, mshindi wa pili Sh 350,000 na mshindi wa tatu Sh 150,000 katika kila mbio kwa wanaume na wanawake ambao walitengewa Sh 10 milioni.
Waandaaji walitenga Sh 34.6 Milioni za zawadi kwa washindi wote wa msimu huu kwenye mbio za uwanja na barabarani za kilomita 10, 21 na 42.