Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafahamu waliochemsha Ligi Kuu Bara

7c6350f33d881bab68a8b316b7bd50cb Wafahamu waliochemsha Ligi Kuu Bara

Sat, 5 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KIPINDI cha usajili huwa kinaendana na mambo mengi mazuri na mabaya, hasa inapotokea mchezaji husika anatakiwa na timu zenye upinzani wa jadi kama ilivyo kwa Simba na Yanga

Kwa Tanzania inapotokea mchezaji huyo akachukuliwa na timu mojawapo na kushindwa kuonesha kile kilichotarajiwa kutokana na tambo zilizokuwa zikitolewa kipindi cha usajili, mambo yanakuwa magumu kwa uongozi na mchezaji husika.

Ipo mifano mingi ambayo imeshawahi kujitokeza katika hilo, lakini leo makala hii inakuletea wachezaji 10, ambao usajili wao uliimbwa sana kwenye vyombo vya habari, lakini wameshindwa kuonesha kile kilichotarajiwa kwa timu zao.

1.Carlos Stenio Fernandes ‘Carlinhos’ – Yanga

Kiungo huyu mshambuliaji raia wa Angola usajili wake ulivuma sana Tanzania na nchi za jirani kutokana na kuwa raia wa kwanza wa Angola kucheza ligi ya Tanzania, huku ikitajwa kwamba amekataa ofa za kwenda kucheza Ureno na kutaka kucheza VPL.

Kuonesha kamba kweli usajili wake ulikuwa niwakipekee, siku alipotua nchini umati mkubwa wa mashabiki wa Yanga ambao haujawahi kujitokeza kwa miaka ya karibuni walijitokeza kumpokea kutokana na imani kubwa waliyokuwa nayo juu yake, kwamba huenda akachangia kurudisha furaha Jangwani.

Matokeo yake imekuwa tofauti msimu unaelekea kwisha mchezaji huyo amecheza mechi 10 za ligi amefunga mabao matatu tu na tayari amevunja mkataba na timu hiyo kwa madai familia yake haina furaha na mambo mengi, ikiwemo lugha na vyakula.

2. Charles Ilamfya- Simba

Huyu ni mmoja wa washambuliaji wazawa aliyesajiliwa mapema na klabu ya Simba akitokea KMC, hiyo ilitokana na watani zao Yanga nao kutajwa kuifukuzia saini ya mshambuliaji huyo, lakini mara baada ya kusajiliwa Chris Mugalu na kufanya vizuri kwa Meddie Kagere na John Bocco, kulimpoteza kabisa Ilamfya.

Kufanya vizuri kwa nyota hao matokeo yake Ilamfya, alijikuta akipata nafasi kwenye mechi za kirafiki na baada ya kuona mambo magumu zaidi kipindi cha dirisha dogo, aliomba kuondoka na uongozi wa klabu ya Simba ukamruhusu kurudi kwenye timu yake ya KMC.

3.Ally Niyonzima- Azam FC

Kuna uwezekano mkubwa uongozi wa Azam ukamruhusu kiungo huyo raia wa Rwanda kuondoka kutokana na mchango mdogo ndani ya timu yao, Niyonzima ni mmoja wa wachezaji ambao walisajiliwa kwa mbwembwe nyingi baada ya kuikataa ofa aliyokuwa amepewa na Yanga.

Tangu uwepo wa kocha Aristica Cioaba hakuwa kipaumbele kwenye kikosi cha Azam, hali hiyo imeendelea hata sasa, ambapo kikosi hicho kipo chini ya Mzambia George Lwandamina, ambaye amekuwa akiwatumia zaidi David Brayson na mkongwe Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

4.Hassan Ramadhani Kessy- Mtibwa Sugar

Licha ya kuwa na uzoefu wa kutosha na Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lakini Kessy amejikuta katika wakati mgumu baada ya kushindwa kuisaidia Mtibwa Sugar timu anayoichezea kwa mara ya pili akitokea Nkana FC ya Zambia alikokuwa akicheza soka la kulipwa.

Kwenye kikosi cha Mtibwa Kessy ni mchezaji wa kawaida na hakuna mchezaji anayetishika naye licha ya kwamba amecheza soka kwenye timu zote kubwa za Tanzania Simba na Yanga na kwenda nje na ukitaka kuamini hilo Mtibwa ni miongoni mwa timu zilizopo kwenye hali mbaya na huenda zikashuka daraja uwepo wake haujakuwa msaada kwa timu hiyo yenye historia kubwa Tanzania.

5. Vitalis Mayanga- Kagera Sugar

Pamoja na uwezo mkubwa aliouonesha akiwa na Ndanda FC hata kuzivutia baadhi ya timu ikiwemo KMC, ambapo alikwenda na kufeli Vitalis, ameshindwa kuisaidia Kagera Sugar kiasi kwamba makocha wamebidi kuweka nguvu kwa kinda Eric Mwijage anayecheza nafasi yake.

Ukifuatilia tangu ajiunge na Kagera Sugar mwanzoni mwa msimu huu, Vitalis amefunga mabao mawili tu na kutoa idadi kama hiyo ya pasi zilizozaa bao, wakati wa usajili wake kocha Mecky Maximo na mashabiki wa Kagera walikuwa na imani kubwa juu ya ujio wake lakini imekuwa tofauti.

6. Adam Salamba- Namungo FC

Salamba alianza msimu huu akiwa ndani ya kikosi cha Namungo na kocha Hitimana Thiery aliyependekeza usajili wake alikuwa na matumaini makubwa na mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba na Stand United, lakini mambo yamekuwa tofauti na matarajio ya wengi.

Mpaka sasa ligi inaelekea ukingoni, Salamba hajawa na kiwango bora na mechi nyingi amekuwa akitokea benchi mbaya zaidi mshambuliaji huyo hajaifungia timu yake hata bao moja kwenye mashindano yote inayoshiriki.

7. Rashid Mandawa - JKT Tanzania

Unaweza kusema mambo yamekuwa magumu kwake pengine kutokana na timu aliyojiunga nayo ambayo haina mwenendo mzuri msimu huu, Mandawa ni miongoni mwa washambuliaji waliopewa nafasi kubwa ya kuipigania JKT Tanzania baada ya kujiunga nayo kwenye dirisha dogo akitokea KVZ ya Zanzibar.

Mchezaji huyo hajaonesha maajabu yoyote mpaka sasa cha zaidi watu wamemkumbuka Adam Adam, mshambuliaji ambaye msimu huu alionesha moto mkali katika kucheka na nyavu.

8.Michael Sarpong- Yanga

Pamoja na kupewa nafasi kubwa ya kuibeba Yanga katika ufungaji nyota huyo raia wa Ghana amekuwa sawa na kazi bure, kwani zile sifa zilizowashawishi mabosi wa Yanga kumsajili hajazionesha hata robo.

Sarpong ameichezea Yanga zaidi ya mechi 20 kwenye mashindano yote lakini amefunga mabao matano tu kinyume na matarajio ya wengi, ikiwemo viongozi wa timu yake ambao huenda msimu unaokuja wakamwonyesha mlango wa kutokea licha ya kusaliwa na mwaka mmoja kwenye mkataba wake.

9.Ibrahim Amme-Simba

Huyu ni mmoja wa walinzi hodari ambao walijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Coastal Union, lakini kukosa uzoefu na ubora wa viwango waliokuwa navyo Pascal Wawa na Joashi Onyango, vimemfanya beki huyo kusota benchi.

Tangu ajiunge na Simba, Amme amecheza mechi tatu pekee za ligi na muda mwingi amekua mtazamaji au benchi kutokana na kiwango chake kutomshawishi bosi wa sasa, Didier Gomes

10. Waziri Junior – Yanga

Kujiunga na Yanga kwake ilikuwa ni bahati ya pekee, lakini bahati mbaya kwake ni kwamba hana upepo wa kuchezea timu kubwa, alishindwa kutamba akiwa na Azam na sasa kuna kila dalili ya kushindwa akiwa na Yanga.

Katika msimu huu mzima akiwa na Yanga, Wazir amefunga bao moja katika mechi zote zikiwemo na zile za kirafiki, mchezaji huyo ameonesha kupoteza hali ya kujiamini iliyosababishwa kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya kikosi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz