Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wavunja ukimya utovu wa nidhamu Ligi Kuu

44922 Pic+nidhamu Wadau wavunja ukimya utovu wa nidhamu Ligi Kuu

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya kuripotiwa taarifa za utovu wa nidhamu kwa wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wadau wa michezo wametoa maoni tofauti kuhusu mwenendo wa tabia hiyo iliyoanza kuota mizizi.

Kauli za wadau zimekuja baada ya picha za mkanda wa video zikimuonyesha mchezaji wa Alliance Juma Nyangi akimfanyia vitendo vya udhalilishaji beki wa Yanga, Gadiel Michael.

Nyangi alionekana akifanya kitendo hicho katika mchezo wa Ligi Kuu ambao Yanga ilishinda bao 1-0, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Hii si mara ya kwanza kwa matukio ya udhalilishaji kuonekana katika mkanda wa video hatua ambayo imewaibua wadau wa michezo wakiwemo wataalamu wa saikolojia ambao wamesema matukio ya aina hiyo yana athari kubwa kwa jamii.

Akizungumza kwa simu jana, mtaalamu wa saikolojia na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St Augostino (SAUT), Leons Maziku alisema matukio ya udhalilishaji wa wachezaji viwanjani yana nafasi kubwa ya kuiathiri jamii wakiwemo watoto. Maziku alisema idadi kubwa ya watoto wamekuwa wakiangalia mpira kupitia televisheni, hivyo wanapoona matukio yasiyofaa kwa jamii yanayofanywa na wachezaji huathirika kisaikolojia.

“Kama mchezaji ana watoto, mke au familia anakuwa katika kipindi kigumu na asipokuwa makini kuna uwezekano mkubwa akashindwa kuendelea kucheza mpira,” alisema Maziku.

Alisema chanzo cha kushamiri matukio ya vitendo vya utovu wa nidhamu, vinechangiwa na baadhi ya wachezaji kutokuwa na ufahamu wa sayansi ya mpira na wanacheza soka kwa kutumia vipaji.

Mtaalamu mwingine wa saikolojia, Modesta Kimonga wa Chuo cha Elimu Patandi Tawi la Tanga alisema mchezaji aliyefanyiwa tukio la udhalilishaji ndani ya uwanja ana nafasi kubwa ya kutoka mchezoni.

“Pia inatoa picha mbaya kwa jamii, hata watoto wanaoangalia mpira wakikutana na tukio la aina hiyo linawaathiri na bahati mbaya mtoto anapoona vitendo vibaya vinadumu kichwani mwake kuliko vizuri,” alisema Kimonga.

Anasema kisaikolojia kuna uhusiano mzuri kati ya mwili na akili, hivyo mchezaji aliyefanyiwa vitendo vya udhalilishaji uwanjani anavurugwa kisaikolojia.

Nahodha wa Azam Aggrey Morris alisema matukio ya aina hiyo yanapaswa kukemewa vikali na vyombo vinahusika na ametoa rai kwa wachezaji wanaodhalilisha wenzao wachukuliwe hatua kali ili kukomesha matukio hayo.

Mchezaji wa Kagera Sugar, Jerry Tegete alisema soka ni mchezo wa kiungwana na ameshauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchukua hatua.

Kocha Fred Felix ‘Minziro’ alisema matukio ya udhalilishaji kwa wachezaji yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara viwanjani na huo ni utovu wa nidhamu unaopaswa kudhibitiwa.

Beki Juma Nyoso aliwahi kuonekana katika picha za mkanda wa video akimdhalilisha John Bocco misimu kadhaa iliyopita.

Katika hatua nyingine, timu ya taifa ya Tanzania kwa vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys imeanza vibaya michuano ya Uefa Assist baada ya kuchapwa bao 1-0 na Guinea mjini Antalya, Uturuki.



Chanzo: mwananchi.co.tz