Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau waitabiria makubwa Yanga

Ad608d173ac46d8bde5f1acacf5a8c63.png Wadau waitabiria makubwa Yanga

Sun, 11 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KILE alichokisema Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi hivi karibuni kuwa Yanga mpya yenye ubora inakuja msimu ujao, kimeungwa mkono na wadau mbalimbali wa soka na kuitabiria makubwa baada ya klabu hiyo kuingia mkataba wa mabilioni na Azam Media.

Alhamisi ya wiki hii Yanga iliingia mkataba wa miaka 10 na Azam Media wenye thamani ya sh. Bilioni 41 pamoja na VAT kwa ajili ya kurusha maudhui na matukio mbalimbali ya klabu hiyo.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema uwekezaji iliopata Yanga unaonesha wazi mapinduzi ya mpira wa miguu yanavyokua kwa kasi.

Miongoni mwa wadau hao ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah aliyesema kwa uwekezaji huo Yanga itapiga hatua kubwa ya kimaendeleo na kuwa miongoni mwa timu hatari kama tu itafanya maboresho ya kikosi chao.

“Ni uwekezaji mzuri kwa Yanga utawasaidia kutimiza ndoto zao lakini pia ni mapinduzi makubwa katika mpira wa miguu nchini,”alisema.

Alisema uwekezaji huo unavutia hata wengine wanaotaka kuwekeza watajitokeza kwa wingi kwa kuwa Azam Media imetoa somo kwa kuinua soka la Tanzania.

Kwa upande wake, Mwanachama wa klabu hiyo Mohamed Msumi alisema “nategemea mengi makubwa yanakuja Yanga , niombe wanayanga utulivu, maendeleo hayaji kwa siku moja,”

Msumi alisema kilichofanywa na Yanga ni kizuri na anatarajia wengi wataiga kwasababu ni jambo la maendeleo.

Katibu Mkuu wa zamani wa TFF Celestine Mwesigwa alisema anaona mpira wa Tanzania ukisogea mbele.

Alisema ana imani Yanga itakuwa miongoni mwa timu zenye ubora na zenye ushindani kwani fedha watakazopata zitawasaidia kutengeneza kikosi kizuri chenye ushindani.

Mshauri wa klabu hiyo Senzo Mbatha alisema uwekezaji huo utasaidia klabu kunuifaka kwani watapata wachezaji wenye kiwango cha juu.

“Ni maendeleo makubwa sio tu kwa klabu yetu bali soka la Tanzania, kwasababu Yanga itasajili wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kushindana kimataifa na kupiga hatua kubwa,”alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz