Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadai riadha wamuunge mkono Filbert Bayi mashindano yake Taifa

A93fb8309ec6e71bc8592e64db19bd13 Wadai riadha wamuunge mkono Filbert Bayi mashindano yake Taifa

Sat, 18 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MASHINDANO ya taifa ya riadha yatafanyika Septemba 5 na 6 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushirikisha karibu mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

Mashindano haya husimamiwa na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), lakini kwa takribani miaka minne hayakuwahi kufanyika kwa sababu wanazozijua wao viongozi wa shirikisho hilo.

Kama fedha walikuwa wakipewa na wadhamini wao hapa nchini pamoja na Shirikisho la Dunia la Riadha (WA), ambalo limekuwa likitoa fedha za msaada na zingine, ambazo pamoja na mambo mengine walitakiwa kuzitumia kwa ajili ya mashindano ya taifa ya riadha.

Kuelekea mashindano hayo ya taifa ya riadha, mikoa inatakiwa kuendesha mashindano hayo na kualika hata mikoa mingine ili kupata au kuchagua wanariadha watakaounda timu ya mkoa.

Hata hivyo, mikoa mingine imekuwa ikibabaisha katika uteuzi wao huo wa timu zao za mikoa kwa ajili ya mashindano ya taifa, kwani wamekuwa wakitaja wanariadha hata bila ya kuandaa mashindano na kuiita timu hiyo ni ya mkoa.

Katika kuonesha njia, mwanariadha wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Filbert Bayi ameamua kuandaa mashindano ya kujipima nguvu, ambayo hushirikisha wanariadha wa Pwani na Dar es Salaam ili kuwapima viwango vyao kabla ya mashindano ya taifa.

Kwa mujibu wa makocha wa riadha akiwemo Ron Davis, ambaye alikuwa kocha wa Bayi wakati akivunja rekodi ya dunia ya mbio za meta 1500 kule Christchurch, New Zealand mwaka 1974, mashindano hayo ya mchujo ni muhimu sana kwa wanariadha kupima viwango vyao.

Hilo ni kweli kwani wanariadha walifanya vizuri katika mchujo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja huo wa Taifa, Dar es Salaam mapema Julai.

Haitashangaza kuona wanariadha wa Pwani, wengi kutoka shule za Filbert Bayi wakifanya vizuri zaidi katika mashindano hayo ya taifa, kwani tayari wameanza kuonesha mwelekeo mzuri chini ya kocha wao, Davis.

Pongezi kwa Bayi ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiupigania mchezo huo ili angalau Tanzania iweze kurejea katika makali ya miaka ya nyuma wakati yeye (Bayi) akivunja rekodi ya dunia. Ni mipango mizuri ya Bayi, lakini inatakiwa kuungwa mkono na vyama vya mikoa au hata taifa (RT) ili kuhakikisha majaribio kama hayo yanafanywa Tanzania nzima na kusaidia kuibua na kuinua vipaji vya wanariadha wetu, ambavyo viko vingi sana nchini.

RT mnatakiwa kuunga mkono jitihada kama hizo, ambazo zinafanywa na wadau wa riadha katika mikoa mbalimbali nchini ili kuurejesha mchezo huo

kileleni wakati Tanzania ilipokuwa ikitamba kimataifa.

Wadau wa riadha sio tu viongozi au mashabiki wa mchezo huo, ila hata taasisi za umma na binafsi, ambazo nazo zinaweza kujitokeza na kuunga mkono mpango huo wa Bayi wa kuendesha mashindano hayo ya majaribo pamoja na vitu vingine vya kuuendeleza mchezo huo.

Pia kufanyia majaribio kwenye Uwanja wa Taifa, hiyo itasaidia sana kuwapa uzoefu wanariadha, ambao ni watoto kuzoea hali ya uwanja huo, ambao sehemu yake ya kukimbilia ni tatan, ambayo wanariadha wengi huwatoa ushamba.

Chanzo: habarileo.co.tz