Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji watano wanaotajwa kuwa wabinafsi zaidi duniani

Serytry Wachezaji watano wanaotajwa kuwa wabinafsi zaidi duniani

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: BBC

"HAKUNA 'mimi' katika timu" ni moja ya kauli ya kizamani sana katika soka. Ni kweli pia kwani, mara nyingi, kila mtu lazima atekeleze sehemu yake kwa matokeo na kwa uboreshaji wa timu.

Akiwa maarufu kwa mbinu zake na kasi dimbani, Arjen Robben alikuwa mmoja wa wachezaji wenye ubinafsi zaidi katika kikosi cha Bayern Munich kwa takriban muongo mmoja.

Lakini nyingi Robben alionekana akitumia mguu wake wa kushoto na kupiga shuti kali kutoka eneo la hatari, badala ya kumpasia mchezaji mwenzake aliyekuwa kwenye eneo zuri. Mwaka 2012, Robben alielezea katika mahojiano, "Ubinafsi ni ubora."

Kawaida, wachezaji wenye ubinafsi wanaweza kuwa wapiga chenga na washambuliaji mahiri - kama Robben, lakini ubinafsi wao unaweza kuwakasirisha wachezaji wenzao.

Wakati mwingine, wanaweza kufidia ubinafsi wote kwa kufunga bao zuri.

Ubinafsi bado ni ubora, angalau kwa baadhi ya wachezaji wa soka la kisasa. Ingawa nyota hawa wamejikusanyia mashabiki kwa umaridadi wao na uzuri wa mtu binafsi. Baada ya yote, hakuna kinachowaudhi mashabiki na wachezaji wenzake kuliko mchezaji mbinafsi ambaye ana siku mbaya mbele ya goli.

Hapa tunawaangalia wachezaji watano wenye ubinafsi zaidi katika soka duniani, twende sasa...

#5. Vinicius Junior | Real Madrid

Vinicius ana sifa zote nzuri ambazo mchezaji mwenye ubinafsi anahitaji ili kufanikiwa. Ana uwezo wa kubadilika, ana kasi na ana uwezo wa kuwakimbia wapinzani na kuwapita. Ingawa Vinicius ameisaidia timu yake kwa kutoa pasi chache za mabao, uchezaji wake wa kusisimua na uthabiti katika kutafuta kupiga shuti unamfanya nyota huyo kuwa mchezaji mwenye ubinafsi.

Lakini Vinicius hana ujuzi kabisa wa kucheka na nyavu. Msimu huu, amepiga takriban mashuti matano kwa kila mechi wakati wa mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Ulaya, na amefunga mara mbili pekee. Uchezaji na ubinafsi wote huo kwenye mpira hautafanya kitu kizuri kama nyota huyo mchanga wa Real Madrid atashindwa kuongeza idadi ya mabao. Ikiwa ataboresha juu ya hili, Vinicius atakuwa nyota halisi katika maamuzi.

#4. Zlatan Ibrahimovic | AC Milan

Zlatan Ibrahimovic alifurahia kiwango bora zaidi cha maisha yake ya soka wakati alipokuwa Paris Saint-Germain, alipotoa pasi za mabao 13 katika msimu mmoja wa ligi.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 40, ana mabao 565 aliyofunga katika michezo 954 tangu Septemba 1999 alipoanza kucheza kule Malmö na leo hii yupo AC Milan.

Wakati alipokuwa Manchester United, wachambuzi wa soka akiwamo Gwiji wa Liverpool, Phil Thompson walimtaja nyota huyo kuwa "mbinafsi sana."

Thompson alisema: "Alikuwa akipiga mashuti 15 katika mchezo na kulikuwa na watu wengine katika nafasi nzuri zaidi." Lakini Ibrahimovic hakukerwa na shutuma kama hizo, akieleza: "Je, nina ubinafsi? Lazima niwe, kuna wafalme wengi lakini kuna Mungu mmoja tu na ni mimi."

#3. Mohamed Salah | Liverpool

Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah kwa sasa yuko katika kilele cha juu kabisa. Mabao kumi na kutoa pasi za mwisho tano katika mechi tisa pekee za Ligi Kuu England kunathibitisha kwamba Salah hazuiliki.

Ingawa kiwango chake kimewafanya 'Wekundu' hao kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi, ubinafsi wake umekuwa ukipigiwa zaidi kelele. Kwenye Ligi Kuu England, Salah amekuwa na wastani wa kupiga mashuti manne kwa kila mchezo, akifunga mara moja kila baada ya mashuti manne.

Wachezaji watatu wa mbele katika klabu ya Liverpool wana uwiano mzuri katika suala la ubinafsi na kutokuwa na ubinafsi.

Miaka michache iliyopita, Sadio Mane na Salah walitawala mitandaoni baada kukwaruzana. Salah alikimbia kwenye eneo hatari na kwenda mwenyewe kufunga badala ya kumpasia Mane, ambaye alikuwa peke yake kwenye nafasi nzuri ya kufunga. Salah alikosa nafasi hiyo.

Hivi majuzi, Gwiji wa Liverpool, Graham Souness, alimwelezea Salah kama, "mchezaji mbinafsi zaidi ambaye nimewahi kumwona."

#2. Cristiano Ronaldo | Manchester United

Muite utakavyo, kipaji cha Cristiano Ronaldo uwanjani na kujituma kwenye mchezo hakuna kifani. Ameitwa mbinafsi, mwenye ubinafsi, na hata mwenye majivuno. Lakini nyota huyo wa Ureno amekuwa na tabia ya kuwajibu wakosoaji wake kwa kufunga mabao mengi zaidi uwanjani.

Akiwa Real Madrid na Juventus, Ronaldo alikuwa na wastani wa kupiga mashuti saba kwa dakika 90. Ronaldo amekuwa akikosolewa mara kwa mara na wachambuzi wengi na hata wachezaji wenzake kwa hili pia. Akiwa Juventus, Antonio Cassano alimkosoa mchezaji huyo, akieleza: "Siku zote amekuwa mbinafsi. Hajali kama wengine wanafunga. Haishi kwa ajili ya soka, anaishi kwa mabao yake mwenyewe, hilo ni wazi."

#1. Neymar | Paris Saint-Germain

Neymar alikuja kujulikana na Klabu za Ulaya wakati akionyesha kiwango cha juu zaidi kule Santos. Muda wake Barcelona na sasa akiwa na PSG haujakuwa tofauti sana.

Mtindo wake wa uchezaji wa Amerika Kusini ulitoa uwiano mzuri kwa Lionel Messi na Luis Suarez pale Barcelona. Lakini, mashabiki wengi wa Ufaransa na wachambuzi hulalamika kila mara kuhusu Neymar.

Bila shaka, mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil ni mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani, na mabao yake ya pekee ni ya ajabu. Hata hivyo, ubinafsi wake na mpira unaweza kuwa chanzo cha kufadhaika kwa wachezaji wenzake, pamoja na watazamaji na wachambuzi.

Mwezi uliopita, Kylian Mbappe alikiri kulalamika kuhusu ubinafsi wa Neymar kwa Idrissa Gueye. Kocha wa PSG Mauricio Pochettino hatimaye alilazimika kuwaweka pamoja wote wawili wakati wa mazoezi ili kuhakikisha anamaliza mzozo wao.

Chanzo: BBC