Baada ya ushindi wa jana wa goli 1-0 dhidi ya Singida United, klabu ya Simba kesho Mei 14, 2018 imealikwa bungeni kwa lengo la kuhudhuria shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupewa pongezi za kutwaa ubingwa msimu wa 2017/18.
Klabu hiyo ambayo asubuhi ya leo imeondoka mkoani Singida na kwenda jijini Dodoma ambapo leo Mei 13, 2018 inachuana na Dodoma Combine kwenye mchezo wa kirafiki, inatarajiwa kesho asubuhi kuhudhuria bungeni.
“Jumatatu tutakuwa bungeni na kesho (leo) baada ya mchezo Wabunge wamewaandalia wachezaji wa Simba karamu kabla ya kesho kwenda bungeni kwenye mualiko.“amesema Haji Manara wakati akizungumza na waandishi wa Habari jana Mei 12 mjini Singida baada ya mchezo dhidi ya Singida United.
Hii sio timu ya kwanza kufanya hivyo, hata mahasimu wao klabu ya Yanga walishawahi kufanya hivyo ambapo mara nyingi huwa kunakuwa na shangwe za kutosha wachezaji wanapowasili bungeni.