Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji Simba wapigwa chini Taifa Stars

14546 Pic+stars TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wachezaji wa Simba waliokuwa wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars', wameondolewa katika kikosi hicho baada ya kushindwa kuwasili kambini kwa wakati.

Wachezaji hao ni pamoja na John Bocco 'Adebayor', Shiza Kichuya, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Hassan Dilunga  na Shomari Kapombe.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wilfred Kidau, amesema Kocha, Emmanuel Amunike, amefanya maamuzi hayo baada ya kushangazwa na jinsi ambavyo wachezaji wa Tanzania wamekuwa wakijivuta wanapoitwa timu ya taifa.

"Niliongea na kocha jana (Jumanne) baada ya kuona wachezaji wa Simba walivyoipotezea Taifa Stars, walitakiwa kuingia kambini jana lakini mchezaji pekee aliyekuwa amefika ni Aisha Manula kitu ambacho ni cha kushangaza,"alisema Kidau ambaye pia aliichezea Simba miaka ya nyuma.

Kidau alifunguka na kusema, licha ya kupokea taarifa hiyo aliamua kumshawishi Amunike aongeze muda mpaka leo Jumatano saa kumi na mbili asubuhi, lakini bado wachezaji hao hawakufika.

"Niliongea na baadhi ya wachezaji wa Simba na kuwaelezea hali halisi lakini kinachoonyesha walikuwa hawajapata taarifa mapema licha ya sisi kupeleka barua,  uamuzi wa mwalimu tunauunga mkono kwa sababu timu ya taifa inahitaji maandalizi na hakuna mtu ambaye yupo juu yake," alifafanua.

Aliongeza na kusema,  baada ya wachezaji hao kuondolewa mwalimu ameamua kuwaongeza wacheza wengine ili kuziba nafasi.

Walioongezwa ni Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Paul Ngalema na Ally Abdukadir (Lipuli FC), David Mwantika na Frank Domayo (Azam FC), Kelvin Sabato na Salum Kihimbwa (Mtibwa Sugar).

Wachezaji wa Azam ndiyo walikuwa wa kwanza kuwasili kambini na wale wa Yanga wanatarajiwa kujiunga na Taifa Stars pindi tu watakaporejea kutoka Rwanda ambako wana mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika na Rayon Sports.

Wachezaji wanaocheza soka ya kulipwa nje ya nchi, wanatarajiwa kuingia kambini Septemba 4, mara tu watakapomaliza majukumu ya klabu zao.

Taifa Stars inajiandaa na mchezo dhidi ya Uganda 'The Cranes' wa  kuwania kufudhu fainali za AFCON Septemba 9.

Chanzo: mwananchi.co.tz