Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji Serengeti Boys mzuka, lengo kubakisha kombe

49830 SB+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Zimebaki siku 13 kabla ya kuanza kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (Afcon U 17) zitakazoanza Aprili 14 hadi 29 jijini Dar es Salaam.

Katika fainali hizo, timu nne zitakazofuzu kucheza nusu fainali zote zitafuzu kuiwakilisha Afrika kwenye Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana zitakazofanyika Brazil baadaye Oktoba.

Wawakilishi wa Tanzania, timu ya vijana ya Serengeti Boys ni kama wametanguliza mguu mmoja kucheza Fainali za Kombe la Dunia kutokana na mzuka ambao vijana wako nao, Spoti Mikiki imezungumza na mchezaji mmoja mmoja na hii ndiyo mipango yao ya Afcon.

Jina: Bernard Castory

Umri: Miaka 16

Nafasi: Fulubeki

Alikotoka: Benard alishauriwa na rafiki yake akajiunge na Akademia ya Marsh ya Mwanza na hapo ndipo safari yake kisoka ilipoanzia.

“Nilikuwa na miaka 12, lakini kocha aliniamini na kunipa unahodha pia akanipandisha hadi U-15, Azam mwaka 2016 walikuja kusaka vipaji wakanichukua na mwaka uliofuatia ndipo kocha Mirambo akaniita timu ya vijana,” anasema.

Matarajio yake kwenye Afcon anasema: “Tumejiandaa kisaikolojia na tumefanya maandalizi ya kina kuhakikisha kombe linabaki nyumbani, Watanzania wajitokeze kwa wingi kutusapoti na sisi vijana wao hatutowaangusha.

Jina:Pascal Msindo

Umri:Miaka 15

Nafasi :beki wa kushoto

Alikuwa mchezaji wa timu ya Mkoa wa Morogoro akitokea Shule ya Msingi Mwande kwenye mashindano ya Umitashumta Taifa mwaka 2017 na huko ndiko alikutana na kocha Mirambo.

“Niliitwa kwenye majaribio Dar es Salaam na hapo ndipo nilipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Serengeti Boys baada ya kufuzu.

“Tumejipanga kupambana, tunahitaji kuwa vijana wa mfano katika soka la Tanzania, kikubwa ni Mwenyezi Mungu atupe afya njema kwenye mashindano hayo ili tutimize ndoto yetu na tufuzu kucheza kombe la dunia,”.

Jina:Alphonce Mabula

Umri:Miaka 15

Nafasi: Beki wa kulia

Alphonce anayetokea mkoa wa Mara alipata ofa ya masomo katika shule ya Sekondari Alliance ya jijini Mwanza kutokana na kipaji chake cha soka.

“Tulichaguliwa katika mashindano maalumu ya kupata vijana wa Serengeti, tuliwekwa kambini tukawa tunafundishwa na kocha Kim (Poulsen) na Mirambo.

Matarajio yangu ni kwamba “Tunataka ubingwa hilo liko wazi, tunajua kucheza nyumbani ni faida ya kwanza, lakini pia tumefanya maandalizi ya kutosha ili kutwaa ubingwa, Watanzania watuombee na sisi hatuwezi kuwaangusha.”

Jina: Ladack Juma

Umri: Miaka 16

Nafasi anayocheza uwanjani: winga

Ladack kwa mara ya kwanza aliitwa Serengeti Boys mwaka 2015 baada ya kung’ara kwenye mashindano ya Umitashumta akiwa na timu ya mkoa wa Morogoro.

“Nilipata nafasi ya kusoma Alliance baada ya kuniona kwenye Umitashumta,” anasema.

Matarajio yangu: “Kwa nafasi yangu nitapambana na kushirikiana na wenzangu kuhakikisha tunafuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia, tunaomba sapoti ya Watanzania, tutapambana kwa nidhamu ya hali ya juu ili tushinde.”

Jina:Erick Boniface

Umri: Miaka 16

Nafasi: winga

Erick aliibuliwa kwenye mechi ya kirafiki kati ya timu yake ya Kigoma iliyokwenda Mwanza kucheza na Alliance na hakurudi na wenzake Kigoma baada ya Alliance kuvutiwa na kipaji chake na kumchukua.

2015 ndipo alijiunga na Serengeti Boys baada ya kuwa miongoni mwa nyota waliochaguliwa katika mchujo uliofanyika Mwanza ukishirikisha timu za mikoa yote.

Matarajio yake kwenye Afcon anasema: “Tutafanya makubwa na kuweka historia ya kwanza kwa Tanzania ya kucheza Kombe la Dunia, binafsi niko vizuri, hamasa kwa wachezaji ni kubwa, uwezo na nia ya kushinda tunavyo hivyo tusubiri siku ifike.”

Jina:Morice Abraham

Umri:Miaka 16

Nafasi: Mshambuliaji

Morice alianza kucheza soka katika timu ya New Talent ya Tabata, Dar es Salaam kabla ya kushiriki mashindano yaliyofanyika uwanja wa Karume, yalipo Makao Makuu ya TFF akiwa kwenye kikosi cha kombaini ya Ilala.

“Baada ya yale mashindano, tulichaguliwa vijana 22 tukaenda kambini kwenye Kituo cha Alliance lakini tulichunjwa na kubaki saba ambao tulijumuishwa kwenye timu ya Serengeti Boys.

“Matarajio yangu kwenye Afcon ni makubwa, tunajua ni mashindano magumu na kila nchi inahitaji ushindi, tutapambana kuipigania nchi yetu, lakini pia kuweka rekodi ya kufanya vizuri katika Afcon,” anasema.

Jina:Kefa James

Umri:Miaka 16

Nafasi: Kiungo mshambuliaji

Kefa alianza soka akiwa shule ya Sekondari Msimbazi na alikutana na kocha Mirambo kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Makongo.

“Alini‘pointi’ katika wachezaji anaowahitaji, lakini taarifa zangu hazikumfikia, hivyo sikuchukuliwa hadi nilipokutana naye tena kwenye mchezo wa kirafiki na Azam ndipo akachukua taarifa zangu na kuniita kwenye timu ya Serengeti, lakini pia Azam baada ya ile mechi walinichukua,” anasema.

Matarajio yake kwenye Afcon anasema: “Kikubwa ni Watanzania watuamini na sisi tutawathibitishia tunaweza kwani malengo na kucheza Fainali za Kombe la Dunia.”

Jina: Rabin Sanga

Umri:Miaka 15

Nafasi: Kiungo mshambuliaji

Rabin alianzia soka kwenye timu ya Bom Bom ya Kariakoo na alikuwa mchezaji bora wa mashindano ya Ndondo Cup Academy.

“Baada ya yale mashindano nilikwenda Uturuki kwenye majaribio, niliporejea ndipo kocha Mirambo aliniita,” anasema.

Matarajio yake kwenye Afcon 2019 anasema huu ni mwaka wa Watanzania kuwa na furaha na kujivunia timu zao hivyo wanafikiria kuendeleza furaha hiyo wa kufuzu kucheza kombe la dunia,” anasema.

Jina: Said Abdallah Zanda

Miaka: 17

Nafasi: Winga

Zanda ambaye ni mzaliwa wa Morogoro aliibukia katika akademi ya Moro Kids ambayo ipo mkoani Morogoro na inasifika kwa kutoa wachezaji wengi wakiwamo, Shomari Kapombe, Aishi Manula na Juma Abdul.

“Serengeti Boys walikuja Morogoro kucheza dhidi ya Akademi yangu ya Moro Kids ndipo wakaniona na kuchukuana. Nakumbuka ilikuwa 2015,” alisema.

Zanda alisema kujiunga katika kikosi hicho kinachonolewa na Oscar Milambo kumemwezesha kujua namna ambavyo mchezaji anatakiwa kuishi katika maisha ya soka.

“Nimejifunza vitu vingi sana katika maisha ya Serengeti nikiwa kama mchezaji, lakini kubwa zaidi ambalo najivunia ni kutengeneza jina (profile) kwasababu kuwa hapa sio jambo ambalo kila mchezaji anaweza kuwapo”.

Zanda anasema jambo ambalo anataka kuhakikisha linafanikiwa ni kuisaidia timu ifanye vizuri katika Fainali za Afcon, baada ya hapo mengine ndiyo yatafuata.

“Naomba Mungu nifanye vizuri katika Afcon ya vijana ambayo tunashiriki. Tukifanya vizuri katika mashindano haya bila shaka hata mimi nafasi ya kucheza nje ya nchi itakuja, kwahiyo kikubwa ni kupambana.”

Aliongeza kwa mazoezi ambayo walikuwa wanafanya pamoja na Mashindano waliyokuwa wanacheza anaamini kabisa watawapa wapinzani wao tabu.

Jina: Arafat Hussein

Nafasi: Beki wa kati

Umari: Miaka 16

Arafat mwenye umbo kubwa linaloonyesha kabisa kwamba yupo tayari kwa mapambano, aliliambia Mwanaspoti kama asingekuwamo katika Akademi ya JK basi angeisikia Serengeti kwenye bomba.

“Nakumbuka nilikuwa tu nacheza mtaani lakini mwaka jana (2018) nilikwenda kujiunga na JK, hapo ndiyo wakaja Serengeti kucheza nasi, kiukweli nilipambana sana na baada ya mchezo niliitwa na nikazungumza na mwalimu.”

Baada ya hapo ndiyo nikachukuliwa na kujumuishwa katika kikosi cha taifa na ninaendelea kuwapo japo nipo chini ya Akademi yangu kama kawaida.

Baada ya Serikali kuonyesha kuhitaji timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Afcon, hata kwa upande wa Arafat napo ni hivyo hivyo baada ya kuweka wazi malengo yake.

“Watanzania watarajie mazuri kutoka kwetu katika fainali hizi, tunajua kabisa kwamba baada ya timu kufanya vibaya Uturuki waliumia, lakini hilo lisiwakatishe tamaa, tutapambana.”

Jina: Ally Hamis Rutinga

Nafasi: Beki wa kati

Umri: Miaka 16

Rutibinga aliibikia Michezo ya Umisseta ndiyo ilianza kumwonyeshea njia ya mafanikio ya mpira kwani, baada ya kushiriki, taa ya kijani ndiyo ikamuwakia.

“Nilikuwa sijamaliza shule bado kwahiyo nikaenda Umisseta, baada ya michezo kwisha nikaitwa kufanya majaribio na baada ya majaribio nikajumuishwa kikosini. Nakumbuka ilikuwa 2016”.

Aliongeza kwa kusema kuwa muda alikoaa katika kikosi hicho amejifunza namna ya kuishi na watu katika mazingira yoyote, kitu ambacho awali kilikuwa kikimsumbua.

“Hapa nimekutana na watu mbalimbali lakini kubwa zaidi nimejifunza maisha ya mpira zaidi, kuna utofauti mkubwa wa maisha ya mpira hapa na huko nyuma nilipokuwa.”



Chanzo: mwananchi.co.tz