Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waamuzi janga jipya Ligi Kuu Bara

14300 Pic+waamuzi TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati maumivu ya Ligi Kuu Tanzania kukosa mdhamini mkuu hayajapoa, kiwango duni cha uchezeshaji kwa baadhi ya waamuzi kwenye mechi za mwanzo kimeanza kutoa taswira mbaya kwa muelekeo wa mashindano hayo msimu huu.

Ligi Kuu haijafikisha raundi tatu, lakini hofu ya mechi za mashindano hayo kutokutoa matokeo sahihi imeanza kutanda baada ya kuibuka makosa yanayotokana na uzembe wa baadhi ya waamuzi kwenye idadi kubwa ya michezo ya raundi mbili za mwanzo.

Michezo minne iliyohusisha timu za Biashara United, Yanga, Mtibwa Sugar, Coastal Union, Mwadui FC, Singida United, Ruvu Shooting na KMC imeshuhudia waamuzi wakikataa mabao halali huku pia ‘wakiua’ mashambulizi ya timu kwa kigezo cha kuotea.

Majanga hayo yalianzia kwenye mechi baina ya Yanga na Mtibwa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini ambapo mwamuzi Meshack Suda na msaidizi wake Godfrey Msakila walikataa bao la mpira wa kichwa la mshambuliaji Herietier Makambo wakidai ameotea.

Kama hiyo haitoshi, mwamuzi wa pembeni namba moja, Sylvester Mwanga alinyoosha kibendera kuashiria Ismail Aidan wa Mtibwa ameotea alipokuwa akielekea langoni mwa Yanga ingawa kwa uhalisia kiungo huyo alipokea mpira akiwa eneo sahihi na hakuotea.

Wakati mjadala wa makosa ya waamuzi wa mchezo baina ya Yanga na Mtibwa ukiwa unaendelea, mechi tatu za raundi ya pili zilizochezwa juzi ziligubikwa na uamuzi ambao ulionekana kuzikandamiza baadhi ya timu na kuzinufaisha nyingine.

Katika mchezo kati ya Biashara na Coastal Union uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, juzi Jumamosi, mwamuzi Nassoro Mwinchui alikataa bao halali lililotokana na mkwaju wa faulo uliopigwa na Biashara na kumgonga mchezaji wa Coastal kabla ya kuingia wavuni, baada ya mwamuzi msaidizi Abdallah Rashid kunyoosha kibendera cha kuashiria ameotea.

Mwadui nayo ilijikuta ikiachiwa maumivu na mwamuzi Ahmada Simba na msaidizi wake Jamada Ahmada ambao walikataa bao la kusawazisha wakidai mfungaji alikuwa ameotea wakati alitokea nyuma ya ukuta wa Singida United kabla ya kufunga.

Kama hiyo haitoshi, mwamuzi Athumani Senkala na msaidizi Nicolaus Makaranga walikataa bao la mshambuliaji Fully Maganga wakidai aliotea, ambalo pengine lingeifanya Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC.

Kama ilivyokuwa kwa Mwadui, Maganga hakuwa ameotea alipofunga bao hilo katika mchezo huo uliomalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1.

Meneja wa Biashara United, Amani Josiah ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi kuchukua hatua mapema kwa waamuzi wanaofanya makosa ili wasivuruge mashindano hayo.

“Inawezekana wanafanya makosa hayo sio kwa sababu ya kuhongwa fedha, lakini pengine ni udhaifu wao wa kutafsiri sheria msimu huu kuna kundi kubwa la waamuzi wapya limeingia kwenye ligi.

Hata hivyo ni vyema hili suala likashughulikiwa kwa haraka kwa sababu waamuzi wachache wanaokosea wanasababisha kuchafua taswira ya ligi, shirikisho na kusababisha watu waanze kuhusisha na masuala ambayo hayana uhusiano wowote kama hilo la kukosekana kwa mdhamini mkuu wa ligi,” alisema Josiah.

Kocha wa Ruvu Shooting, Abdulmutick Haji alisema ni vyema waamuzi wakaongeza umakini kwa sababu udhaifu wao unaziumiza timu zilizotumia gharama kubwa kufanya maandalizi.

“Haifurahishi kwa kweli inaumiza kwa sababu tunapambana kusaka ushindi lakini mtu mmoja anasababisha tukose pointi tatu ambazo tulistahili kupata.

Tumefunga bao halali ambalo halina utata lakini limekataliwa jambo ambalo sio mara ya kwanza kutokea. Nadhani waamuzi wanapaswa kuchezesha mechi kwa umakini kwa sababu makosa yao yanazigharimu timu,” alisema Haji.

Hata hivyo, uzembe wa waamuzi wa mechi hizo umeishitua TFF ambayo imeamua kuwasimamisha waamuzi wote waliolalamikiwa na imepanga kuwachukulia hatua.

“Ni kweli tumepokea malalamiko kuhusu baadhi ya waamuzi kuchezesha chini ya kiwango baadhi ya michezo ya ligi. Kimsingi lengo letu tunataka tuwe na ligi bora hatuwezi kuacha hilo lipite.

Kwa kuwa ligi inaendeshwa kwa kanuni, jambo la kwanza tulilofanya ni kuwasimamisha waamuzi hao halafu baadaye, kamati ya uendeshaji wa ligi (Kamati ya saa 72) itatangaza hatua zaidi watakazochuliwa iwapo uchunguzi utabaini walifanya makosa kwa mujibu wa sheria,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama.

Chanzo: mwananchi.co.tz